Kwa Hili la Mwanamuziki Diamond, Basata Mnajitukanisha Wenyewe

BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata) chini ya katibu mkuu wake, Godfrey Mngereza, ni kama limepoteza mwelekeo. Viongozi wake wamekuwa na ndimi mbilimbili, maamuzi yao hayana nguvu tena na hata umuhimu wake wa kuwepo, haupo.


Ukitazama sarakasi zinazoendelea kati ya Basata na wasanii Nasibu Abdul (Diamond Platnumz) na Raymond Mwakyusa (Rayvanny), kuhusu kufungiwa kwa wimbo wa Mwanza (Nyegezi), unaweza kuwafananisha Basata na mbwa mkubwa asiye na meno, anaishia kubweka tu lakini hawezi kung’ata.

 Novemba 12, 2018 (mwezi uliopita), Basata walitangaza kuufungia wimbo wa Mwanza (Nyegezi) wa Rayvann na Diamond Platnumz. Wakati Basata wakitangaza kuufungia wimbo huo kwa sababu za kimaadili, hatua hiyo ilikuwa imekuja kwa kuchelewa.

 Unafungiaje wimbo ambao tayari watu wameshaudownload, watu wanao kwenye simu zao, kwenye laptop zao, kwenye vyombo vyao vya usafiri mpaka majumbani mwao? Licha ya kutangaza kuufungia wimbo huo, na kuwakataza wasanii husika kutoupiga sehemu yoyote, wimbo uliendelea kuwa maarufu mitaani, na Rayvanny na Diamond, kwa kiburi cha kuona Basata ni sawa na mbwa anayebweka tu lakini asiyeweza kung’ata, wakaendelea kuupiga kwenye shoo za Wasafi Festival.

 Japokuwa wengi waliliona tukio la wasanii hao kupafomu wimbo huo uliofungiwa kwenye shoo yao ya Mwanza, ukweli ni kwamba wimbo huo pia ulipigwa kwenye Wasafi Festival Zanzibar. Pengine Basata hawakuwa wakijua, au walijua lakini wakaamua kulinyamazia tukio hilo. Pengine hata ishu ya kupafomu wimbo huo Mwanza, kama isingeshikiwa bango na vyombo vya habari, Basata wangeendelea kulala usingizi wa pono kwa sababu hawafuatilii, hawajui kinachoendelea kwenye shoo za wasanii huko mikoani.

 Nilitegemea siku ileile wimbo huo ulipopigwa Zanzibar, Basata wangechukua hatua lakini walipiga kimya mpaka wasanii hao walipokuja kurudia kitendo hicho jijini Mwanza. Yote tisa, kumi ni tukio la kuwafungia wasanii hao kufanya matamasha ndani na nje ya nchi baada ya kudharau amri ya Basata ya kuufungia wimbo huo. Wajuzi wa mambo, kuanzia siku hiyohiyo ya kutolewa kwa barua hiyo, walianza kutoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanachokifanya Basata ni kama kujitekenya na kucheka wenyewe kwa sababu ukweli ni kwamba wanajua hawana uwezo wa kusimamia amri yao.

 Hawana uwezo wa kumzuia Diamond na wenzake kufanya shoo. Siku chache baadaye, wakati Basata wakiwa wanaendelea kushikilia msimamo wao, Diamond alifanya mkutano na
waandishi wa habari nchini Kenya na kueleza kwamba walishamalizana na Basata na wameruhusiwa kufanya shoo hizo, kila mmoja akabaki na mshangao.

 Ili kuua soo, Basata wakaja na tamko lingine la kusisitiza kwamba hawajawasamehe Diamond na wenzake na kuwaonya eti waache kusambaza taarifa za uongo. Watu wakazidi kupatwa na mshangao, Diamond anapata wapi jeuri ya kusema wameshamalizana na Basata wakati anajua kwamba siyo kweli? Wenye uelewa wa mambo wakajua lazima kuna kitu nyuma ya pazia.

 Kilichotabiriwa na wengi ndicho kilichotokea, siku kadhaa baadaye, katika barua iliyosainiwa na Mngereza, Basata eti waliamua kuwaruhusu Diamond na wenzake waendelee na shoo zao za nje ya nchi kwa kisingizo kwamba wakati wanawafungia, tayari wasanii hao walikuwa wameshasaini mikataba ya kufanya shoo hizo.

 Unajiuliza, wakati Basata wanatoa amri yao, hawakulijua hilo? Unajiuliza pia, kwa nini Basata wamekuwa na ndimi mbilimbili katika hili? These guys are not serious! Wanajitukanisha wenyewe kwa kukosa msimamo, tutegemee wasanii wengi zaidi kuendelea kuwaonesha dharau za waziwazi kama alivyofanya Diamond na wenzake.

Za Chembe Lazima Ukae HASH POWER, +255 719 401 968

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Basata weka faini kubwa ya kutisha kudhibiti maadili. Je inaweza kuwa sheria? Ili iwe msumeno?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad