Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ni miongoni mwa viongozi watakaokwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho Ijumaa Desemba 21, 2018 kusikiliza kesi inayowakabili vigogo wa Chadema, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Desemba 20, 2018 na mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Itifaki, Mawasiliano wa Chadema, John Mrema inaeleza kuwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye naye atakuwepo.
Mrema amesema viongozi watakaokuwepo mahakamani ni wa vyama sita vilivyofanya mkutano juzi visiwani Zanzibar na kutoa maamuzi mawili mazito.
Mkutano huo ulioratibiwa na CUF chini ya Maalim Seif, vyama hivyo viliazimia kuanza kufanya mikutano ya hadhara kwa kuwa ni haki yao kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.
Pia, vilitangaza rasmi kwamba wanasiasa wote waliopo jela kwa tuhuma za kisiasa hao ni ‘Wafungwa wa kisiasa’ na kuanzia sasa wataitangazia dunia hivyo.
Maamuzi hayo ya Zanzibar yalisainiwa na Maalim Seif, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia; mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi; naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu; mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Kesi hiyo ya jinai inayowakabili viongozi hao itatajwa kesho mahakamani hapo wakati Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Esther Matiko wakisubiri hatima ya rufaa yao.
Mbowe na Matiko wako gereza la Segerea, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana Novemba 26, 2018 kwa kukiuka masharti ya dhamana ikiwemo kutoka nje ya nchi bila kibali.
Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicenti Mashinji; manaibu katibu mkuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).
Wengine ni mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; mbunge Tarime Vijijini, John Heche.
Mbowe na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka 12 ikiwemo kuandamana bila kibali, mkusanyiko usiokuwa wa halali pamoja na kutoa lugha za uchochezi.
Lowassa, Zitto Kabwe na Maalim Seif kutinga mahakamani kesho
0
December 21, 2018
Tags