Lugola Awataka Polisi Kuimarisha Ulinzi Msimu Wa Sikukuu.....Aagiza Vibaka, Matapeli Na Majambazi Wakamatwe

Lugola Awataka Polisi Kuimarisha Ulinzi Msimu Wa Sikukuu.....Aagiza Vibaka, Matapeli Na Majambazi Wakamatwe
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amelitaka Jeshi la Polisi nchini liimarishe ulinzi wakati wa sikukuu za krismasi na mwaka mpya na kuwataka wananchi kutokujisahau kwasababu ya sikukuu hizo.

Akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kisorya, Kata ya Kisorya, Jimbo la Mwibara, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara, Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, alisema msimu huu wa sikukuu vibaka, majambazi na matapeli hutumia sikukuu hizo kufanya uhalifu.

Alisema Polisi wanapaswa kujipanga zaidi ili kuhakikisha sikukuu hizo zinasherekewa kwa amani kwa kufanya ulinzi kona zote za nchi ili wananchi waweze kufanya shughuli zao kwa usalama na kuendelea kuijenga nchi yao.

“Hili tatizo la kuwepo vibaka na kuwafanya wananchi waishi kwa wasiwasi nchini, sasa napenda niwaambie nyie wananchi wa hapa Kisorya, na Tanzania kwa ujumla, Jeshi lipo imara, hao vibaka pamoja na majambazi wote, sasa hawana nafasi, nawaagiza polisi kufanya msako mkali kuwakamata matapeli, vibaka na majambazi wanaojitokeza hasa kipindi hiki cha maandalizi za sikukuu za krismasi na mwaka mpya, “ alisema Lugola.

Pia Lugola aliwataka wananchi watoe taarifa polisi iwapo wataona dalili zinazoashiria uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ili Jeshi la Polisi liweze kuzifanyia kazi mapema taarifa hizo.

Aidha, Lugola aliwataka Polisi nchini kuwakamata watu wanaowarubuni wanafunzi pamoja na kuwatia mimba, wawafungulie mashtaka haraka iwezekanavyo kutokana na tatizo hilo kushika kasi nchini na kuwafanya wanafunzi kukatisha masomo yao.

“Wananchi wa Kisorya, tatizo hili ni la nchi nzima, na mara kwa mara nalikemea na kuwapa maagizo polisi kuwakamata watu wanaoharibu watoto wadogo wa shule kwa kuwatia mimba, nawataka polisi muwe wakali sana kuhusu hilo, hakuna kucheka na mtuhumiwa, kamateni wekeni rupango na apelekwe mahakamani mtuhumiwa ili kukomesha tatizo hili sugu hapa nchini,” alisema Lugola.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, alikiri tatizo hilo kuwa sugu wilayani humo, hata hivyo alimuahidi Waziri Lugola watalishughulikia na wahalifu wote watakamatwa.

“Mheshimiwa Waziri, matatizo ya wananfunzi kutiwa mimba hili lipo wilayani hapa, ila siku za nyuma tuliwahi kumkamata mwalimu ambaye alimtia mimba mwanafunzi na baadaye akasingizia kuwa mimba hiyo siyo yake na alipigwa na mwanafunzi mwenzake, hivyo tupo wakali kuhakikisha tunalimaliza tatizo hilo kwa kuwakamata na kuwapeleka mahakamani watuhumiwa,” alisema Bupilipili.

Pia katika mkutano huo, Waziri Lugola aliwataka wananchi wa jimbo lake waanze maandalizi ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kuepuka janga la njaa lisije likawakumba endapo hawatalima. Hata hivyo, kijiji hicho alichokitembelea, kwa mujibu wa taarifa ya mipango yao ya kilimo walisema kuwa wana upungufu mkubwa wa mbegu za mazao mbalimbali hasa zao la pamba.

“Nimeagiza maafisa ugani waje kuangalia upungufu wa mbegu za pamba na kutatua kero hii kutokana na taarifa yenu ya mpango wa kilimo ya mwaka 2018/2019, na pia nasisitiza zaidi mlime mazao ya chakula kwa wingi,” alisema Lugola.

Lugola anaendelea na ziara jimboni kwake akisikiliza kero za wananchi pamoja na kuhamasisha kilimo cha mazao ya pamba, mahindi, mpunga, viazi na mengineyo ambayo wakazi wa jimbo lake wanalima mazao hayo kwa wingi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad