WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka wananchi wenye sifa ya kupata Vitambulisho vya Taifa nchini waende kujisajili katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho hivyo (NIDA) zilizopo katika Wilaya wanazoishi kwakuwa ni lazima kila Mtanzania awe nacho.
Lugola alisema wapo wananchi ambao hawakujitokeza wakati usajili ulipokua unafanyika katika mitaa na vijiji vyao, na pia wapo ambao kipindi hicho walikua na miaka 17 na kukosa sifa ya kujisali, lakini kwasasa wamefikisha miaka 18, nao wanapaswa kufika ofisi za wilaya ili wapate huduma hiyo ya usajili.
Akizungumza na wananchi wa Mji wa Kibara, Jimbo la Mwibara, Bunda, Mkoani Mara, Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, alisisitiza kuwa, zoezi la kujisajili si la kupuuziwa kwa kuwa ni lazima kila mwananchi raia wa Tanzania awe na kitambulisho cha Taifa.
“Vitambulisho hivi ni muhimu kuwa navyo, nawaomba Watanzania msipuuze hili zoezi, na pia napenda kusisitiza kwa mara nyingine muelewe vizuri kuwa vitambulisho hivyo vitatolewa kwa watanzania wenye sifa tu ambao watapita katika mchujo ili kuepusha kutoa kwa wasio raia,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa, NIDA ipo makini na pia watahakikisha kuwa wanasajili wananchi nchi nzima kwa umakini na pia kutoa elimu zaidi kuhusiana na kuwa na kitambulisho hicho kwasababu kuna baadhi ya watanzani bado hawajajua umuhimu wa kuwa na kitambulisho cha taifa.
“Ndugu wananchi wa hapa na Watanzania kwa ujumla, naomba ieleweke kuwa, hakuna mwananchi mwenye sifa atakayekosa kitambulisho cha taifa, kikubwa fuateni utaratibu baada ya kwenda Wilayani mkipata maelezo kabla ya kuanza kujisajili ikwemo pamoja na hatua zote mtakazo pitia mpaka mnakipata vitambulisho hivyo,” alisema Lugola.
Alisema moja ya hatua wanazozipitia Maafisa wa NIDA ni pamoja na utambuzi wa watu gani wanaweza kupata vitambulisho hivi, na pia katika utambuzi wanapaswa kuwa makini sana kwasababu wasijesije kupenyeza wasiokuwa raia na baadae zoezi hilo likaja kuwa gumu.
Lugola alisema baada ya hatua ya utambuzi, inafuata hatua ya usajili ambayo pia hatua hiyo nayo inahitaji umakini mkubwa zaidi na ikimalizika hatua hiyo majina yaliyosajiliwa yanarudishwa tena kwa wananchi kuulizwa kama waliosajiliwa wanatambuliwa katika sehemu wanazoishi, hatua hiyo ikiwa na lengo la kupata taarifa sahihi ya waliosajiliwa wanatambuliwa au hawatambuliwi na wazawa katika eneo husika.
“Endapo majina tulioyasajili na kuyaleta kwenu, nanyi mtayakataa basi hatutaweza kutoa vitambulisho kwa huyo au hao mliowakataa, na endapo mtayaridhia majina tuliyowaletea, basi tutaweza kuwatengenezea vitambulisho bila shaka yoyote, na endapo kuna mwananchi amekataliwa na Kijiji kuwa hatambuliwi, anayohaki ya kukata rufaa na kutueleza kwanini apewe kitambulisho,” alisema Lugola.