Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa la Croatia Luka Modric ameshinda tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka 2018, na kuwa mchezaji wa kwanza tofauti na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kushinda tuzo hiyo baada ya miaka 10.
Modric, 33, ameshinda kombe la Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei kwa mara ya tatu mfululizo na kulisaidia taifa lake kufika hatua ya fainali katika michuano ya Kombe la Dunia.
Mchezaji wa zamani wa Brazil na AC Milan Kaka, alishinda tuzo hiyo mwaka 2007, na baada ya hapo Messi na Ronaldo wameshinda mara tano kila mmoja tuzo hiyo ya thamani kabisa kwa wachezaji wa kandanda duniani.
Ronaldo, ambaye amehamia Juventus msimu huu amemaliza katika nafasi ya pili mwaka huu, huku Messi akishika nafasi ya tano. Nafasi ya tatu ameshika mshambuliaji wa Atletico Madrid Antoine Griezmann huku mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe akishika nafasi ya nne - wawili hao walikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichoshinda Kombe la Dunia mwaka huu.
Huu umekuwa mwaka wa kutuzwa kwa Modric ambaye awali alishinda tuzo ya FIFA ya mchezaji bora wa kiume na pia alishinda tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Dunia.
Akiongea na BBC, Modric amesema tuzo yake ni zawadi kwa wachezaji wote ambao waliikosa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
"Labda huko nyuma kuna wachezaji ambao walistahili kushinda Ballon d'Or kama Xavi, Andres Iniesta au [Wesley] Sneijder lakini sasa watu wameamka a wanaanza kuangalia wachezaji wengine," amesema.
"Huu umekuwa mwaka wa kipekee sana kwangu. Ni vigumu kuzielezea hisia zangu kwa maneno. Ni kitu cha pekee sana kwangu."
Modric amewasifia Ronaldo na Messi kama "wachezaji bora kabisa", na kuongeza "hivyo ushindi wangu huu unamaanisha kuwa nimefanya vitu vikubwa sana uwanjani mwaka huu, na ndio maana 2017-18 umekuwa ni mwaka wangu."
Modric ndiye mchezaji bora wa kiume wa Fifa
Goli la Pavard ndilo bora zaidi Kombe la Dunia 2018
Mohammed Salah ndiyo mchezaji pekee kutoka Afrika aliyeingia katika 10 bora kwa kushika nafasi ya sita, na ndiyo mchezaji kinara kutoka ligi ya premia ya England.
Modric alikuwa ni miongoni mwa wachezaji nane wa Real Madrid kati ya wachezaji 30 waliokuwa wakiwania tuzo hiyo, akiwemo Gareth Bale aliyemaliza katika nafasi ya 17.
Mshambuliaji wa Lyon na Norway Ada Hegerberg, 23, ameshinda tuzo ya kwanza ya Ballon d'Or kwa wachezaji wa kike huku Mbappe,19, akishinda tuzo ya Kopa inayotolewa kwa mchezaji bora chini ya miaka 21 kwa kupigiwa kura na washindi wa zamani wa Ballon d'Or.
10 Bora ya Ballon d'Or
1. Luka Modric (Real Madrid and Croatia)
2. Cristiano Ronaldo (Juventus and Portugal)
3. Antoine Griezmann (Atletico Madrid and France)
4. Kylian Mbappe (Paris St-Germain and France)
5. Lionel Messi (Barcelona and Argentina)
6. Mohamed Salah (Liverpool and Egypt)
7. Raphael Varane (Real Madrid and France)
8. Eden Hazard (Chelsea and Belgium)
9. Kevin de Bruyne (Manchester City and Belgium)
10. Harry Kane (Tottenham and England)
Ballon d'Or ni nini?
Tuzo ya Ballon d'Or imekuwa ikitolewa nchini Ufaransa kila mwaka toka 1956, na msindi wake wa kwanza alikuwa mchezaji kutoka Uingereza Stanley Matthews.
Tuzo hiyo awali ilikuwa ni kwa wachezaji wa Ulaya tu kabla ya kufanyika mabadiliko mwaka 1995 na kujumuisha wachezaji wa mataifa yote duniani, mradi wanasakata kandanda katika vilabu vya Ulaya.
Listi ya majina ya wachezaji 30 bora huandaliwa na baadae kupigiwa kura na wanahabari wa michezo kutoka sehemu tofauti duniani, ambapo kila nchi hupiga kura moja.
Kutoka mwaka 2010 mpaka 2015 tuzo hiyo iliunganishwa na ile ya Fifa lakini zilitengana mwaka 2016 ambapo Fifa ilianza kundaa tuzo zao wenyewe.
Luka Modric Amaliza Ufalme wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo Tuzo ya Ballon d'Or
0
December 04, 2018
Tags