Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuendelea na majukumu yake ya ubunge nje ya nchi yaliyomfanya ashindwe kufika mahakamani leo Desemba 6, 2018 kwa ajili ya kesi ya jinai inayomkabili.
Mdee na viongozi wakuu wa Chadema, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wakikabiliwa na mashtaka 13 ya uchochezi, uasi na kuhamasisha wafuasi wao kutenda makosa, hakuweza kufika mahakamani wakati kesi yao ilipotajwa leo.
Mdhamini wa Mdee, Farws Robson ameieleza mahakama kuwa mbunge huyo hakuweza kufika kwa kuwa yuko Burundi kwa safari ya kibunge akishiriki michezo ya wabunge wanawake wa mabunge ya Afrika Mashariki.
Robson ameieleza mahakama kuwa Katibu wa Bunge alimwandikia barua Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu kuhusiana na safari ya Mdee na kwamba anatarajia kurejea nchini Desemba 20, 2018.
Mbali na Mdee, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ambaye pia ni mshtakiwa katika kesi hiyo hakuwepo mahakamani leo.
Upande wa mashtaka kupitia kwa wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi umeieleza mahakama kuwa hauna pingamizi dhidi ya Mdee kwa kuwa wanayo nakala ya barua ya Bunge kumwombea Mdee ruhusa.
Pia amesema hawana pingamizi dhidi ya Heche kwa kuwa alikuwa na ruhusu hiyo.
Akitoa uamuzi Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri amesema kwa kuwa alipokea nakala ya barua ya Bunge ikimwombea ruhusa Mdee anakubali aendelee na shughuli zake hizo.
Kuhusu Heche amesema pia anamruhusu aendelee na ruhusa yake ya kumuuguza mkewe ambayo alishampatia.
Hata hivyo amewataka wote wawepo tarehe nyingine kesi hiyo itakapotajwa,ameiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 21, 2018.
Mbali na Mdee Mdee, Heche na Mbowe, washtakiwa wengine ni katibu mkuu, Dk Vicent Mashinji; naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Wengine ni mweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.