Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemuachia huru, Mohamed Kiluwa (50) aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kutoa rushwa ya Sh milioni 90 kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kwa sababu ushahidi wa mashtaka ulikuwa wa hisia.
Akisoma hukumu hiyo leo Jumatatu Desemba 24, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo Samuel Obas amesema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukuwa na mashiko kwa sababu umeshindwa kuthibitisha kosa.
"Ushahidi wa upande wa mashtaka umekaa kihisia zaidi, hivyo mahakama yangu imeshindwa kumtia hatiani mshtakiwa, hivyo mahakama hii imemuachia huru Kiluwa" amedai Hakimu Obasi na kuongeza: "Hisia hata kama zina nguvu kiasi gani, haziwezi kufanya mahakama imtie hatiani," amesema Hakimu Obasi.
Amesema kutokana na hali hiyo, mahakama hiyo imemuachia huru na kuamuru fedha zake ambazo ni Sh milioni 90 arudishiwe.
Hata hivyo, ameruhusu upande wa jamhuri kukata rufaa kama hawajaridhika na uamuzi huo.