Kontena lililosheni nywele bandia, mali ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwengelo lipo hatarini kupigwa mnada baada ya kukwama kulipia ushuru bandarini.
Kukwama kwa kontena la Jokate na vigogo wengine kumekuja ikiwa ni takriban miezi mitatu imepita tangu ulipoibuka mjadala uliotikisa ndani na nje ya nchi kuhusu makontena 20 ya samani mbalimbali, mali ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Makonda aliingiza nchini makontena hayo ya samani kutoka kwa Watanzania waishio Marekani, akitumia jina binafsi kwa lengo la kusambaza kwa walimu na baadhi ya shule za jijini Dar es Salaam huku akikataa kulipia ushuru wa zaidi ya sh bilioni 1.2.
Kwa mujibu wa Tangazo la Kamishna wa Forodha na Ushuru, Usaje Asubisye la Desemba 18, ametoa Ilani ya kusudio la kupiga mnada kwa kontena hilo na ya vigogo wengine kwa kushindwa kulipia ushuru hadi siku ya tangazo.
Jokate aliingiza kontena hilo namba HJCU2320135 kupitia kampuni yake ya Kidot ambayo inajishughulisha na mambo ya mitindo na urembo.
Hata hivyo, Jokate alipotafutwa alimtaka Mwandishi kuwasiliana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kidot, aliyemtaja kwa jina moja la Bruce, lakini alipotafutwa na kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS), hakuweza kujibu licha ya ujumbe huo kumfikia.
Mbali ya Mkuu huyo wa Wilaya, yapo Makontena mengine ya vigogo na taasisi mbalimbali ambayo yamepewa siku 30 kulipia ushuru vinginevyo yatapigwa mnada.
Miongoni mwa vigogo hao ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi ambaye ana makontena ya vipuri (spare parts) yaliyoagizwa kwa niaba ya Jeshi la Polisi Tanzania.
Makotenta hayo yamehifadhiwa katika bohari (warehouse) ya TICTS jijini Dar es Salaam moja, likiwa na namba FSCU8360050 na jingine namba CLHU8647166.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Ahmed Msangi alipoulizwa alisema ; “Sina taarifa hizo, waulizeni wao TRA.”
Alipoulizwa, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo alisema walichokifanya ni kutoa notisi ya wahusika kutoa mizigo yao bandarini na hawezi kueleza zaidi.
“Taarifa zaidi zinabaki kuwa kati yetu TRA na mteja,” alisema.
Mbali ya IGP, mali nyingine zilizoko kwenye orodha hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni, ambaye aliagiza kontena lenye vigae vya plas-ki (plascles) likiwa na namba GATU0012947 likiwa limehifadhiwa katika bohari ya Said Salim Bakhresa jijini Dar es Salaam.
Tangazo hilo la kamishna huyo wa forodha na ushuru lilitolewa rasmi kwa umma Desemba 19, mwaka huu likibainisha mali kadhaa kutoka kwa watu, taasisi, mashirika binafsi na madhehebu ya dini zilizoko hatarini kupigwa mnada.
Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Ecobank Tanzania Ltd, Timu ya Soka ya Simba, Kampuni ya Saruji ya Dangote, Kampuni ya Yapi Merkezi Upanga Tanzania inayohusika ka-ka ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).
Nyingine ni kampuni ya Oilcom, Shellys Pharmace-cals, Hospitali ya Tumbi Pwani, Mbeya Cement, Tanzania Commodi-es Trading Co. Ltd, 21 st Century Tex-les – kiwanda cha mfanyabiashara maarufu Mohamed Dewji.
Wengine ni Mohammed Enterprises, GSM Foam Company Ltd, kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Pls na Hospitali ya Agha Khan.
“Umma unatangaziwa kwamba bidhaa zilizoorodheshwa zitatambuliwa kuwa zimetelekezwa katika maeneo mbalimbali ya forodha kama wahusika hawataziondoa katika kipindi cha siku 30 (kuanzia Desemba 19).
"Baada ya kuisha kwa kipindi tajwa, Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa atauza kwa njia ya mnada au kuondosha mizigo hiyo katika maeneo ya forodha kwa namna atakayoona inafaa,” inasomeka taarifa ya kamishna huyo wa forodha wa TRA.
Miezi mitatu iliyopita, Makonda aligoma kulipa ushuru na kujikuta akingia kwenye mzozo na TRA huku akitishia kuwa anatayenunua makontena hayo kwenye mnada, atalaaniwa.
Kauli hiyo ilimuibua Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango ambaye alisisitiza lazima makontena hayo yauzwe kama sheria inavyotaka bila kujali ni mali ya nani.
Mzozo huo ulipigiliwa msumari na Rais John Magufuli ambaye alisema lazima sheria ifuatwe na kuwataka TRA kuendelea kuyapiga mnada makontena hayo.