Marekani Kuondoa Wanajeshi Wake Syria

Marekani Kuondoa Wanajeshi Wake Syria
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jumatano kwamba wanajeshi wa Marekani wataanza kuondoshwa nchini Syria na kurejeshwa nyumbani, kwavile wameshafanikiwa kulitokomeza kundi linalojiita Dola la Kiislam (IS).

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jumatno kwamba wanajeshi wa Marekani wataanza kuondoshwa nchini Syria, kwavile wamefanikiwa kutimiza lengo lao la kulitokomeza kundi linalojiita Dola la Kiislam (IS) na sasa hawahitajiki tena nchini humo.

"Tumekuwa tukipambana kwa muda mrefu sana nchini Syria. Nimekuwa rais kwa zaidi ya miaka miwili. Tumejitahidi sana na tumelishinda kundi la IS. Tumewashinda na tumewashinda vibaya sana. Tumewapokonya ardhi waliokuwa wanidhibiti. Na sasa ni wakati wa wanajeshi wetu kurudi nyumbani," amesema Donald Trump wakati akitangaza uamuzi wake huo.

Uamuzi huo wa kuondoa kabisa wanajeshi wa Kimarekani nchini Syria, umethibitishwa pia na maafisa wa Marekani na unatarajiwa kutekelezwa katika miezi ijayo. Lakini kuondoka kwao huko kunaweza kukafanya vigumu kupambana na kundi hilo iwapo litapata tena nguvu.

Na Marekani pia itapoteza ushawishi wake katika eneo hilo, na kuhujumu juhudi zake za kidiplomasia za kutaka kumaliza vita vya Syria vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vimeingia mwaka wake wa nane.

Maseneta wakosoa uamuzi wa Trump
Uamuzi huo wa Trump umekosolewa na Maseneta pamoja na baadhi ya wanachama wenzake wa chama cha Republican, ambao wanadai kwamba kuondoka kutazipa nguvu Urusi na Iran, ambazo zinamuunga mkono Rais wa Syria Bashar Assad. Maseneta hao wa Marekani ikiwa ni pamoja na wa chama cha Republican Jumatano usiku walimsisitizia Rais Donald Trump kutafakari upya uamuzi wake huo wa kuondoa majeshi ya Marekani kutoka Syria.

Uamuzi huo pia unaweza kuliathiri kundi la muungano wa wanamgambo wa Kikurdi na Kiarabu unaojulikana kama SDF. Kundi hilo limekuwa mstari wa mbele katika kupambana na kundi la IS, lakini sasa linakabiliwa na kitisho kutoka Uturuki, kwa vile taifa hilo linatafakari kufanya mashambulizi nchini Syria.

Makamanda wa jeshi la Marekani waliopo Syria, ambao wamekuwa na uhusiano mzuri na viongozi wa kundi la SDF wameeleza wasiwasi wao juu ya uamuzi huo wa Trump na jinsi utakavyohatarisha vikosi vinavyoungwa mkono na Marekani.

Lakini Trump amesema kwake yeye operesheni ya Syria imemalizika, kwavile wanamgambo wa kundi la IS wameshapoteza maeneo waliokuwa wakiyadhibiti.

Maafisa wa Marekani wamesema wanajeshi wataanza kuondolewa Syria katika siku 60 hadi 100 zijazo na kwamba Wizara ya Mambo ya Nje itaanza kuondoa wafanyakazi wake kutoka Syria katika kipindi cha masaa 24.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad