Masha amiliki asilimia 68 ya hisa kampuni ya Fastjet

Masha amiliki asilimia 68 ya hisa kampuni ya Fastjet
Waziri  wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, amenunua asilimia 64 ya hisa za kampuni ya ndege ya Fastjet Tanzania, hivyo kuongeza hisa zake kufikia asilimia 68 kutoka asilimia nne aliyokuwa akimiliki awali.

Ofisa Uhusiano na Masoko wa Fastjet, Lucy Mbogoro, jana alisema Masha alinunua hisa hizo ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuimarisha na kuboresha kampuni hiyo, kuelekea katika mikakati mipya ya kuboresha huduma inayotarajiwa kuanza mwakani.

Alisema Masha ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet amenunua hisa hizo ambazo ni asilimia 17 zilizokuwa zikimilikiwa na Kampuni mama ya Fastjet PLC ya Afrika Kusini na asilimia 47 ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na wazawa, ikiwa ni hatua ya kuifanya kampuni hiyo imilikiwe moja kwa moja na Watanzania.

“Kwa sasa ieleweke kwamba asilimia 68 ya hisa zote za Fastjet nchini inamilikiwa na Lawrence Masha na thamani halisi ya hisa hizo itatajwa baadaye, baada ya kuweka mambo yote sawa. Ila hii ni sehemu ya kuifanya kampuni hii imilikwe na Watanzania,” alisema.

Alisema ukitoa asilimia 68 ambazo sasa zinamilikiwa na Masha, ikiwa ni kiasi kikubwa kinachotoa nafasi ya umiliki wa kampuni hiyo, asilimia 32 zilizobaki bado zinamilikiwa na Haine Kaizer ambaye ni raia wa Afrika Kusini.

Mbogoro alisema pamoja na kununuliwa kwa hisa hizo, kampuni hiyo yenye ndege mbili kwa sasa ikiwa na safari mbili kila siku kati ya Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro pia safari moja kila siku kati ya Dar es Salaam na Mbeya iko katika mikakati ya kupanua huduma zake kwa kuongeza idadi ya ndege na safari hizo.

Alisema kampuni hiyo ambayo kwa sasa inamiliki asilimia 42 ya soko (kwa mujibu wa ripoti ya robo ya kwanza ya mwaka inayoishia Aprili) pia inatarajia kuongeza safari zake kati ya Dar es Salaam na Harare (Zimbabwe) na Dar es Salaam na Lusaka (Zimbabwe) ambazo zinafanyika mara tatu kwa wiki, pia kuongeza maeneo ya safari za ndani.

Kwa mujibu wa ripoti za umiliki wa soko, kufikia Aprili mwkaa huu Fastjet ilikuwa ikiongoza kwa asilimia 42 ikifuatiwa na Precision Air iliyokuwa ikimiliki wastani wa asilimia 35 ya soko na Air Tanzania ambayo iliongeza wigo wake kutoka asilimia 2.5 mwkaa 2016 hadi asilimia 20 mwanzoni mwa mwaka huu.

Fastjet Tanzania imekuwa kwenye mpango wa kununua hisa zote na kuifanya kuwa kampuni ya Kitanzania baada kampuni ya Fastjet PLC kutangaza kusitisha kutoa fedha kwa kampuni ya Fastjet Tanzania.

Fastjet PLC ni kampuni ya ndege ya kimataifa ikiwa na makao yake Afrika Kusini na Uingereza,i inayofanya pia usafirishaji Afrika kwa kujikita katika utoaji wa huduma kwa gharama ndogo

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad