Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Arusha, Amina Mollel amekana madai ya kumchongea Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari kwa Rais John Pombe Magufuli wakati kiongozi huyo alipokuwa ziarani Mkoani Arusha.
Mbunge Molel ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv na kubainisha kuwa watu ndio ambao walimnukuu tofauti kauli yake ya kulalamikia kutokuwepo kwa Mbunge wa Jimbo husika kwenye mkutano huo badala yake alimaanisha Mbunge, Gibson Blasius Meiseyeki wa Arumeru Magharibi.
"Pale tulipokuwa sisi halikuwa jimbo la Nassari, lilikuwa jimbo la Arumeru Magharibi ambalo ni la Mbunge Gibson, sasa nashangaa watu wamenilisha maneno ambayo sikusema, sikumtaja Nassari wala mbunge wa jimbo japo ni kweli wote hawakuwepo kwenye mkutano," amesema Mollel.
"Niwaulize watu ambao walimtaja Nassari badala ya Gibson lengo lao lilikuwa nini?, kuhusu kutopeleka madai yangu kwenye vyama vyao, nisingeweza kupeleka kwani wao hawajui kama mbunge wao hafiki jimboni, mimi nilimshtaki kwa Rais na Mwenyekiti wangu," ameongeza.
Disemba 02 mwaka huu akiwasilisha maombi kwenye mkutano wa Rais Magufuli bila kutaja jina la mbunge husika, Mbunge huyo alilalamikia kutokuwepo kwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi Gibson Blasius Meiseyeki.