Mbunge wa CHADEMA Aliyepata Ajali Dodoma Ahamishiwa Muhimbili

Mbunge wa CHADEMA Aliyepata Ajali Dodoma Ahamishiwa Muhimbili
Mbunge wa Viti Maalumu, Kunti Majala (Chadema), aliyepata ajali ya gari na kujeruhiwa akiwa na familia yake mkoani Dodoma amesafirishwa kwa ndege kwenda Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Kunti amesafirishwa juzi usiku akitokea Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, akiwa pamoja na majeruhi wengine na kufikishwa moja kwa moja Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na baadae kuhamishiwa Moi.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ilisema Kunti na wenzake walisafirishwa kwa ajili ya matibabu zaidi kutokana na hali zao baada ya kupata ajali hiyo.

“Hadi sasa, watu wawili wa familia yake wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na ajali hii iliyotokea eneo la Chemba, wakati Kunti na familia yake walipokuwa wakielekea Kondoa,” ilielezwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mbali ya mbunge huyo majeruhi wengine ni pamoja na dereva wa gari hilo, Stephen Massawe ambaye pia ni dereva wa Chadema Kanda ya Kati na watu wengine sita, wote ni wa familia yake.

“Tutaendelea kutoa taarifa kwa umma juu ya tukio hilo kadiri itakavyohitajika,” ilisisitiza taarifa hiyo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha amethibitisha kupokewa kwa majeruhi hao.

“Kweli walifikishwa hapa Muhimbili, wamelazwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI),” alisema Aligaesha.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad