Membe ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje na mgombea urais wa mwaka 2015, amesema kuwa amemueleza Dkt. Bashiru siku atakapofika ofisini hapo, pia Cyprian Musiba awepo ili kuthibitisha tuhuma hizo kwani ndiye aliyeziibua kupitia Gazeti lake la Tanzanite.
MEMBE ALONGA HIVI!
Kufuatia taarifa za kwenye mitandao jioni hii na messages nyingi zinazokuja kwangu, nimeamua kutoa ujumbe huu kwa wote wanaonitakia mema.
Usiku huu nimempelekea KM wa Chama chetu ndugu Bashiru ujumbe wa kukubali kumwona mara nitakaporejea kutoka Nje ya nchi.
Nimeshangazwa kidogo na utaratibu uliotumika kuniita, lakini kwa sababu ya ugeni kazini na kwa sababu ninamheshimu, nitakwenda kumwona Ofisini kwake.
Wote tunajua kuwa mwanzilishi wa tuhuma zote dhidi yangu tunazozisoma na kuzisikia kwenye vyombo cha habari na mitandaoni ni Cyprian Musiba.
Nimemwomba Katibu Mkuu Bashiru kuwa siku nitakayokwenda kumwona, Musiba awepo ili atoe ushahidi kwa sababu mtoa tuhuma ndiye mwenye wajibu wa kuthibitisha aliyoyasema. Mimi kama mtuhumiwa siwajibiki kufanya hivyo. Burden of proof ni ya Musiba. Mimi nitajibu mapigo atakapomaliza kutoa ushahidi mbele ya KM.
Aidha nimemwambia KM kuwa nilitegemea kuwa mara baada ya Mwanaharakati Uchwara kushusha tuhuma nzito kwa watu na viongozi wenye historia na heshima kwenye Chama Mimi nikiwemo, Musiba anayelalamikiwa na wengi kuwa ni mwongo, mzushi, mfitini na mtu asiye na heshima, angaliitwa Chama na TISS ili athibitishe madai yake, na aonywe kwa utovu wake wa nidhamu na kwa kuchafua majina ya viongozi.
Hilo halikufanyika na mwanaume kwa kutumwa na kujituma anaendelea kuchafua watu. Mimi niliamua na bado nitaendelea kukaa kimya kwa sababu Chama na vyombo vya Usalama ndiyo vilivyopaswa kumhoji Musiba.
Baada ya kujiridhisha kuwa aliyoyasema yana mshiko, basi kamati ya maadili ya chama ingalifanya kazi ya kuwaita wahusika kwa kanuni na taratibu za Chama chetu na kuwahoji!
Kutokufanya hivyo, nimemwambia KM ndiko kulikotufanya wengine tuanze kuamini kuwa sauti tunayoisikia ni yake Musiba, lakini akili si yake ni ya kupewa na waliomtuma, wanaomlipa na wanaomlinda. Tuhuma nitungiwe mimi, halafu nitakiwe kuzijibu!! Nikaamua kumpuuza na nitaendelea kufanya hivyo. Kumjibu Musiba ni kumpa heshima asiyostahili.
Mpaka hapo nitakapokutana na KM wa Chama chetu na Musiba, tuvute subira! Nawapenda na kuwashukuruni wote mliotaka niseme neno. BM.