MARCUS Onyango mkazi wa Kijiji cha Nyakiswa, Kata ya Kyanyari, wilayani Butiama mkoani Mara amevamiwa na majambazi sita waliokuwa na silaha, wakamjeruhi kwa risasi kisha kumpora fedha na madini ya dhahabu yenye thamani ya mamilioni. Katika tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita, Onyango ambaye ni mfanyabiashara mdogo wa madini, alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake, kisha kuibiwa madini yenye thamani ya shilingi milioni 5 na fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 2.
Akisimulia mkasa huo, Onyango ambaye amelazwa wodi namba 8 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, mjini Musoma akiendelea na matibabu, alisema siku ya tukio majambazi hao walimvamia nyumbani kwake majira ya saa 3:30 usiku.
“Nilikuwa nimelala ndani na mke wangu, majira ya saa 3:30 usiku, wakaanza kugonga mlango , nikawauliza nani wenzangu, wakasema wao ni polisi kutoka kituo kidogo cha Kiabakari. “Nikawauliza mnataka nini? Wakasema wanataka kufanya upekuzi nyumbani kwangu. Nikakataa, nikawaambia kama wanataka kupekua waende kwa kiongozi yeyote wa mtaa waje naye.
“Niliposema hivyo wakabadilisha maelezo, wakasema nifungue mlango haraka, la sivyo watavunja. Wakasema wanataka milioni 50 ambazo wameambiwa eti nimeuza kifusi cha mchanga wa madini,” alisema Onyango. Onyango ambaye alihamishiwa hospitalini hapo baada ya hali yake kubadilika alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama, alisema muda mfupi baadaye majambazi hao walivunja mlango kwa kutumia jiwe maarufu la fatuma na kufanikiwa kuingia ndani.
Mfanyabishara huyo aliyejeruhiwa vibaya na risasi sehemu za mapajani na miguu yake miwili, alisema majambazi hao walivyoingia waliendelea kusisitiza wanahitaji milioni 50 alizouza kifusi cha mchanga wa madini. “Mabishano yalikuwa makali, wao walisema nitoe milioni 50, nikawaambia sina hiyo pesa mle ndani, ndipo wakanipiga risasi mapajani na miguuni kama unavyoona (anamwonyesha mwandishi). Hawakuelewa, waliendelea kusema wanachotaka ni pesa tu,” alisema na kuongeza:
“Walimpiga sana mke wangu (Jestina) kwa mabapa ya mapanga na hatimaye wakafanikiwa kuchukua shilingi milioni 2 na dhahabu zenye thamani ya shilingi milioni 5, vyote vilikuwa kwenye mfuko wa koti langu.”
Anasema walipiga kelele za kuomba msaada lakini majirani walihofia kutoka baada ya kusikia milio ya risasi, hivyo majambazi hao ambao mmoja alikuwa mwanamke walifanikiwa kuwaibia bila kuwa na udhibiti wowote kisha kutokomea kusipojulikana. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Juma Ndaki, ambaye alifika katika eneo la tukio Alhamisi, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa alipokea simu kutoka kwa wasamaria wema usiku wa tukio, ambapo alituma kikosi cha polisi.
“Hilo tukio ni kweli lipo. Nilituma askari usiku uleule, lakini walifika na kukuta tayari majambazi hayo yamefanya uhalifu na kutoweka katika eneo hilo. Bado tunaendelea na msako mkali ili kuwanasa,” alisema Kamanda Ndaki.
Mfanyabiashara Apigwa Risasi na Majambazi Apolwa Mamilioni
0
December 04, 2018
Tags