Mizengo Pinda Ammwagia Sifa Rais Magufuli


Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema Rais John Magufuli ndiye kiongozi ambaye Watanzania walikuwa wanamhitaji kutokana na uthubutu alionao katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo hapa nchini.


Pinda ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 23, 2018 jijini Dodoma wakati akifungua Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Dodoma.


Amesema wakati fulani kwenye uongozi wake wapinzani waliwahi kusema Serikali yao ni dhaifu haina makali hivyo walikuwa wanataka kiongozi mkali na mwenye uthubutu japo kwa sasa tena wameanza kumlalamikia Rais Magufuli ambaye ndiye kiongozi waliyekuwa wanamtaka.


Amesema Rais Magufuli ameweza kutekeleza miradi mbalimbali iliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo Serikali zingine zilizopita zilishindwa kuitekeleza kwa kisingizio cha kuogopa gharama kubwa.


Ameitaja baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa kuzalisha umeme wa Stigler’s Gauge na Serikali kuhamia Dodoma.


Amesema japo agizo la Serikali la kuhamia Dodoma lilianza tangu Serikali ya kwanza lakini lilikuwa gumu kutekelezeka kutokana na kuangalia gharama kubwa ya Serikali kuhamia mkoani hapa kufuatia kutokamilika kwa miundombinu mbalimbali.

 

Akizungumzia suala la watumishi hewa Pinda amesema hata katika uongozi wao liliwatesa hadi wakafikia uamuzi wa kuanza kuwalipa watu mishahara dirishani lakini hawakufanikiwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad