Mtu Mmoja Ajinyonga Nyuma ya Bodi ya Korosho....RPC Atoa Tamko


Baada ya tukio la mtu mmoja kukutwa amejinyonga mtaa wa maduka makubwa mkoani Mtwara, kwenye kichaka kilichopo nyuma ya jengo la Bodi ya Korosho, Kamanda wa Polisi mkoani humo amesema kwamba mpaka sasa tukio hilo halina uhusiano na suala la korosho japo bado uchunguzi unaendelea.


Kamanda wa Polisi, ACP Blasius Chatanda amesema kwamba Marehemu aliyejulikana kwa jina la Mosses Malolela, 'Wadasani' alikutwa amejinyonga saa nane usiku wa Disemba 16 mwaka huu huku kukiwa hakuna ujumbe wowote aliouacha.


Kamanda Chatanda amesema kwamba marehemu Mosses (30), ni mkazi wa Mpwapwa mkoani Dodoma na kwamba bado haijajulikana ni jambo gani ambalo lilimpeleka mkoani Mtwara hivyo bado wanafuatilia.


Akijibu swali la kama marehemu Mosses ni mmoja kati wa wafanyabiashara wa Korosho wasio waaminifu, maarufu kama wanunuzi wa 'Kangomba', Kamanda Chatanda amesema, "Mpaka wakati huu hakuna taarifa zozote ambazo zinahusisha tukio hilo na suala la korosho. 


"Kwa kuwa bado tunaendelea na uchunguzi tutajua sababu za kujinyonga ingawa siku hizi  matukio ya kujinyonga yanasababishwa na mambo mbalimbali yakiwepo msongo wa mawazo, hali ya maisha lakini pia mapenzi nk, japo kwa marehemu Mosses bado hatujafahamu ni nini".


Mwili wa Marehemu Mosses upo katika sehemu ya kuhifadhia maiti mkoani Mtwara baada ya kutolewa juu ya mti ulipokuwa ukining'inia baada ya kujinyonga kwa kutumia waya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad