MVP wa michuano ya Sprite Bball Kings mwaka 2018, Baraka Sadick ameendelea kuonesha ubora wake baada ya kuweka rekodi ya kufunga pointi 72 katika mchezo mmoja kitu ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya mchezo wa kikapu nchini.
Baraka ambaye alikuwa anachezea timu ya mabingwa wa Sprite Bball Kings, Mchenga Bball Kings ameweka rekodi hiyo Katika mashindano ya Taifa Cup yanaoendelea mkoani Simiyu ambayo yamefikia hatua ya fainali na inapigwa kesho ikikutanisha timu anayochezea Baraka ya mkoani wa Dar es Salaam (Dream team) dhidi ya timu ya mkoa wa Mwanza.
Katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya timu ya mkoa wa Mara, Baraka alifunga pointi 72 ndani yake akifunga 'Three point' 17 na kufanya mpaka sasa kwa Tanzania yeye ndio aliyefunga Three points nyingi kuliko mchezaji yeyote.
Pia katika michezo mingine, Baraka amekuwa akiongoza kwa kufunga pointi nyingi hivyo kuendelea kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi wa Kikapu kuwahi kutokea.
Katika mechi dhidi ya Mwanza alifunga pointi 38, Rebound 2 na Assists 3 huku Three pointi zikiwa 3. Dar es salaam iliibuka na ushindi wa pointi 95 kwa 45 za Mwanza.
Mchezaji Baraka Sadick akikimbia na mpira kwenye game 1.ya fainali dhidi ya Flying Dribblers
Katika mechi nyingine dhidi ya Singida, Baraka alifunga pointi 56, Rebound 4 na Assists 9 na Three pointi zilikuwa 11. Dar es salaam ilishinda kwa pointi 171 kwa 29 za Singida.
Kwenye mechi dhidi ya Shinyanga, Baraka alifunga pointi 26, Rebound 1, Assists 3, huku akifunga Three pointi 6, Dar es salaam ikishinda pointi 107 dhidi ya 70 za Shinyanga.
Kabla ya fainali ya kesho itakayopigwa saa 10:00 jioni, Baraka ana wastani yaani 'Avarage' ya pointi 48 kwa kila mchezo na Assists 7 kwa kila game, pia Rebound 2 kwa kila mchezo.