Mwalimu mmoja amepoteza kazi baada ya kuwaambia wanafunzi wake kuwa Santa Claus ama maarufu kama Father Christmas hayupo ulimwenguni.
Mwalimu huyo msaidizi alikuwa akifundisha wanafunzi wa darasa la kwanza huko New Jearsey nchini Marekani.
Santa Claus ama Santa kwa ufupi ni hekaya ya zamani ambayo yadaiwa babu huyo mwenye ndevu nyeupe zinazofika tumboni na ambaye juvalia mavazi ya rngi nyeupe na nyekundu pamoja na kofia huwapatia zawadi watoto watiifu katika mkesha na asubuhi ya siku ya Krismasi.
Mwalimu huyo pia inadaiwa aliwaambia wanafunzi wake wenye miaka sita na saba kuwa hekaya nyengine kama 'Tooth Fairy' na 'Easter Bunny' pia ni za uongo. Easter Bunny ama Sungura wa Pasaka anaaminika kuwapatia watoto wema mayai na zawadi nyengine wakati wa pasaka, nayo huaminiwa sana na watoto.
Father Christmas na Easter Bunny ni hekaya ambazo zinalenga kuwafanya watoto kuwa watiifu na wenye adabu, na kuwaaminisha kuwa ukiwa mkaidi hautopata zawadi itakapowadia siku kuu. Ni sawa na usemi wa waswahili kuwa: 'Makaidi hafaidi mpaka siku ya Idi'.
Tooth Fairy ni hekaya ambayo watoto wanaaminishwa baada ya kung'oa jino endapo wataliweka chini ya mto wa kulalia basi asubuhi hugeuka zawadi na pesa. Lengo ni kuwafanya wasiogope na wawe na hamu ya kung'oa meno ili wapate zawadi.
Kwa mujibu wa maofisa elimu wa jimbo hilo, kitendo cha mwalimu huyo hakikubaliki na kimewaathiri wanafunzi wake.
Afisa elimu wa eneo hilo René Rovtar hakutaja jina la mwalimu huyo aliyefutwa kazi. "Kitendo hicho kimenitesa na kunisikitisha sana, hatafundisha tena hapa," amesema. c
Amesema pia kuna umuhimu mkubwa sana kimaadili kwa watoto kuamini katika hekaya hizo na kisha akapiga picha na Father Christmas na kuirusha kwenye mtandao wake wa Twitter na kuandika kuwa anaamini (kuwa yupo).