MFANYABIASHARA Happy Mboya (38) aliyefariki dunia katika hospitali ya Mwananyamala, Jumapili, Desemba 16 na kupangwa kusafirishwa jana kwenda Moshi kwa mazishi leo, mwili wake umezuiwa kutoka hospitalini baada ya kudaiwa umegundulika kuwa una madawa ya kulevya.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Siyanga alisema jana kuwa Polisi wa Kituo cha Osterbay jijini hapa wamechukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Alisema ameshatuma maofisa wake katika hospitali hiyo ili kufuatilia kwa karibu tukio hilo ikiwa ni pamoja na kupata taarifa za kina ikiwamo aina ya dawa alizomeza na kiasi. Siyanga alisema baada ya uchunguzi kukamilika, atatoa taarifa kamili juu ya tukio hilo. Wakati Siyanga akisema hayo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Muliro alipoulizwa kuhusu suala hilo alitaka apewe muda ili kufuatilia.
“Ndiyo nasikia kwako ila naomba nipe muda nitakujulisha ukweli wa suala hili,” alisema Muliro.
Akizungumza jana, baba mdogo wa marehemu, Ally Bilali alisema baada ya kurejea nchini, Happy alifikia katika nyumba ya kulala wageni ambayo haikufahamika na mtu mwingine isipokuwa mume wake.
“Hata dada yake alikuwa hafahamu kuwa amesharudi kwa sababu alidai kuwa simu yake imeharibika na wasingeweza kuwasiliana kumbe ilikuwa kumficha. Alipata taarifa baada ya mdogo wake kuzidiwa na wahudumu kumpigia simu ndipo alienda kumchukua kumuwahisha hospitalini,” alisema.
Alisema baada ya kufika hospitalini na kupimwa, alionekana kuwa na njaa kali jambo ambalo lilimlazimu daktari kumuandikia dripu za maji ili kumsaidia.
“Lakini hizo dripu hakuwekewa na hatukuambiwa sababu ya msingi hadi alipofariki. Taratibu za kusafirishisha mwili kwenda Moshi zilipofanyika ndiyo tuliambiwa kuwa hatuwezi kutoa mwili kwa sababu una dawa za kulevya.
Alimtuhumu mume wa marehemu kuhusiana na tukio hilo huku akidai kwamba tayari anashikiliwa na jeshi la polisi. Bilali alisema Happy ambaye ameacha watoto wawili, alikuwa mkazi Sinza na mfanyabiashara kati ya India na China. Hata hivyo, hakubainisha aina ya biashara aliyokuwa akifanya katika mataifa hayo.
Mwili wa Mfanyabiashara Wazuhiliwa Mwananyamala Baada ya Kugundulika Una Madawa ya Kulevya
0
December 21, 2018
Tags