Naibu Waziri Wa Fedha Akagua Matumizi Ya Mashine Za EFD Kariakoo


Na Veronica Kazimoto

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, amefanya ziara ya kushtukiza katika maeneo ya Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukagua matumizi ya Mashine za Kielektroniki za EFD.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha ziara hiyo katika maduka mbalimbali, Naibu Waziri huyo amesema kuwa, bado kuna wafanyabiashara ambao hawatoi risiti za EFD na wengine hawatumii kabisa mashine hizo.

“Nimekuwa nikifanya uchunguzi wangu binafsi na wa kiofisi kujiridhisha kama wafanyabiashara wanatoa risiti za kieletroniki na nilichobaini ni kwamba bado kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao hawatoi risiti na wananchi wengi hawaombi risiti za EFD,” alisema Dk. Ashatu.

Dk. Ashatu amebainisha kuwa, alifanya uchunguzi binafsi ambapo alikwenda kama mnunuzi na alipoomba risiti za EFD aliambiwa mashine za kutolea risiti hizo ni mbovu na kupewa risiti za kawaida.

Miongoni mwa wafanyabiashara waliotembelewa na Naibu Waziri huyo ni Faridi Mohamed ambaye ni muuzaji wa Vifaa vya Michezo katika Mtaa wa Lindi eneo la Kariakoo aliyemuuzia Dk. Ashatu bidhaa mbalimbali na kumpatia risiti isiyo ya kielektroni na alipoulizwa alidai kuwa mashine ni mbovu.

Dk. Ashatu hakuridhishwa na majibu hayo na kuamua kufanya ziara kukagua maduka yaliyopo katika maeneo hayo ambapo ametoa wito kwa wafanyabiashara kutoa risiti kila wanapouza bidhaa na huduma mbalimbali na wananchi kudai risiti kila wanapofanya manunuzi.

 Mwisho.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad