Naomba nikualike rasmi siku ya leo tuweze kujifunza kwa pamoja jambo hili la msingi litakalokusaidia kuweza kuishi vyema mwezi huu wa kumi na mbili bila ya kuwa na mawazo lukuki.
Mwezi wa kumi na mbili asikwambie mtu, ni kati ya miezi ambayo huwa ina mambo mengi kidogo kwa upande wa sikukuu hizi zilizopo mbele yetu, hivyo usipokuwa makini utajikuta mwezi huu umekuacha mweupe na hauna kitu. Hivyo unapaswa kuwa makini sana na matumizi yako ya pesa.
Si kila jambo linalokatisha mbele ya mboni ya macho yako ni lazima ununue la hasha, mengine wacha yakupite, nasema hivyo kwa sababu mwezi huu kuna mengi sana yatapita mbele ya macho yako yenye kila aina ya uzuri wa kujiuza hivyo unatakiwa kuwa makini na mambo hayo.
Nakueleza ya kwamba uwe na umakini kwa sababu mwezi wa kwanza unakaribia na huwa una mambo mengi sana ambayo yatakuhusisha wewe kuweza kutoa pesa zako. Mambo hayo ni kama vile ada za wanao, mambo ya kilimo na mambo kama hayo.
Hivyo kama utaponda mali kufa kwaja katika kipindi hiki cha sikukuu basi mwezi wa kwanza utakuwa ni mwezi ambao ni mgumu sana kwako. Hivyo kila wakati unashauriwa ya kwamba si kila kitu ambacho kitapita mbele ya macho ni lazima ununue vingine viache vikupite.
Na. Benson Chonya.