Nape Nnauye: CCM Imevamiwa na Wasaka Tonge

Nape Nnauye: CCM Imevamiwa na Wasaka Tonge
Wakati sakata la Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dr.Bashiru Ally na kada wa Chama hicho, Bernard Membe likiendelea kuchukua nafasi kubwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, mbunge wa Mtama Nape Nnauye ameibuka na kusema CCM imevamiwa na wasaka Tonge wenye maslahi na matumbo yao kuliko chama.

Nape Nnauye ambaye ni mbuge wa Mtama, ametoa kauli hiyo baada ya kuenea kwa taarifa kuhusu madai ya  kuanzishwa kwa chama kipya kitakachoitwa USAWA, ambapo Bernard Membe na Nape Nnauye wametajwa kuwa miongoni mwa watakaotimkia kwenye chama hicho kipya.

Taarifa iliyoandikwa kwenye ukurasa wa facebook unaofahamika kwa jina la "Sauti ya Kisonge" na kuenezwa kwenye mitandao hii leo, inadai Chama hicho kinachotarajiwa kusajiliwa hivi karibuni, kinawahusisha pia  mawaziri kadhaa wa utawala uliopita, mawaziri wanne kutoka Zanzibar  na mabalozi kadhaa wastaafu na waliopo nje.

"Chama Kipya kinachotarajiwa kusajiliwa hivi karibuni kwa jina la USAWA ndio kilichomuhusisha Membe na Nape Mnauye na mawaziri kadhaa wa utawala uliopita na mawaziri wanne wa kutoka Visiwani Zanzibar  mabalozi mbali mbali waliopo nje na Mabalozi wastaafu,Wanajeshi wastaafu na makamanda wa Jeshi la Polisi inasemekana wamekibariki Chama kipya cha USAWA .Kauli za Katibu Mkuu wa CCM Dr Bashiru,na Mpiga debe wa CCM Musiba walianza kupiga kelele baada ya taarifa ya ujio wa chama hichi kipya kilichovutia Wanaharakati wengi wa CCM Wasioridhishwa nchi inavyoendeshwa" imesomeka taarifa hiyo.

Sasa baada ya kuenea  kwa taarifa hizo mbunge wa Mtama Nape Nnauye, ameibuka na kujibu tuhuma hizo, kuwa yeye bado yupo sana CCM na kwamba wanaosambaza taarifa za uongo ndio ambao wataondoka na kumuacha yeye ndani ya chama.

Kauli hiyo ya Nape, ameitoa kupitia akaunti yake ya twitter, ambapo ameiita taarifa hiyo kuwa ni ya kipuuzi na iliyojaa uongo.

"Niliposoma upuuzi huu sasa ninaamini CCM imevamiwa na wasaka tonge wasio jua imani wala itikadi ya chama,hawana wanachokiamini isipokuwa matumbo yao,uongo huu ni kwa faida ya nani? watatoka wao,wenye chama tupo sana"umesomeka ujumbe huo.

Huu unakuwa ujumbe wa tatu kutoka kwa Nape Nnauye tangu kuanza kwa mjadala wa Membe ambapo juzi aliweka picha ya pundamilia wakinywa maji na kuandika maneno yaliyoashiria kutounga mkono kwake kwa kinachoendelea ndani ya chama.

"Mkinywa maji ya mto mmoja si busara kuyatibua maji kwa miguu kwani wote mtakunywa Maji machafu! Yanini kutibua maji bila sababu!?" Aliandika Nape kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Nape hakuishia hapo, jana pia kupitia ukurasa wake wa Twitter, akaweka picha ya Mzee Kinana (Katibu mkuu aliyepita wa CCM) akiwa amebeba jembe begani na akaandika;

"🚶🏾‍♂️🚶🏾‍♂️🚶🏾‍♂️🚶🏾‍♂️🚶🏾‍♂️shambani tu! "

Hii si mara ya kwanza kwa Nape Nnauye kuhusishwa na kuasisi vyama vyenye mrengo huo, ikumbukwe mwaka 2010 kiliibuka chama kilichoitwa Chama Cha Jamii (CCJ) ambapo Nape, Mwakyembe na Marehemu Samwel Sitta walitajwa kukiasisi ingawa wenyewe walikanusha.

Mara kadhaa Nape Nnauye amekuwa akikosoa wahamaji wa vyama wanaohama vyama vyao kwenda CCM, akisema hawana itikadi ya chama hicho bali huwa wanahama kufuata maslahi na vyeo.

Kauli ya Nape inakuja sambamba na ile ya Katibu Mkuu wa CCM,  Dk Bashiru Ally ambaye naye amelikana andiko  linalosambaa mtandaoni likionyesha kuwa ameendeleza mjadala unaomuhusu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Dk Bashiru amesema andiko hilo si lake na hayupo katika mfumo wowote unaomuwezesha kuwasiliana kupitia mitandao ya kijamii zaidi ya kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno.

Sehemu ya andiko hilo linalosambaa kwenye mitandao ya kijamii linasema,

 “Zipo taarifa kwamba yupo kiongozi mmoja aliyewahi kuwa mwandamizi wa Taifa hili eti kanikosoa kuhusu utaratibu niliotumia kumwita ndugu Membe, mimi niombe hawa wastaafu watulie ili tukiweke chama sawa...Na nirudie tu kusema ndugu Membe kama atakuwa hajafika ofisini kabla ya tarehe 17 na 18, 2018 nitakiomba kikao cha kamati kuu ya NEC kimwazimie.”

Dk Bashiru amesema waliofanya hivyo ni wale waliozoea kuendesha nchi kiholela na bado watazua mengi.

 “Watu wanaonijua wanafahamu jinsi ninavyotumia simu, sipo huko na  sina Instagram, Twitter, WhatsApp, Facebook wala mfumo wa barua pepe kwenye simu yangu, ni wazushi hao puuzeni hizo habari, ”amesisitiza

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad