Polisi nchini Sudan wamewatimulia mabomu ya machozi mashabiki wa mpira mabao walikuwa wakiandamana kutaka kung'atuka kwa rais Omar al-Bashir.
Maandamano yaliyoanza wiki iliyopita yametanda nchi nzima huku waandamanaji wakitaka kuondoka kwa raisi huyo aliyedumu madarakani kwa miaka 29.
Mamia ya waandamanaji walizuia barabara moja iliyokaribu na uwanja wa mpira katika mji mkuu wa Khartoum, siku ya Jumapili kisha kukabiliana na polisi wa kutuliza ghasia.
Viongozi wa upinzani wanadai watu 22 wameuawa toka Jumatano ya wiki iliyopita, lakini viongozi wa serikali wanadai idadi hiyo imetiwa chumvi.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita bei ya baadhi ya bidhaa muhimu zimeongezeka mara mbili nchini Sudan huku mfumuko wa bei kufikia asilimia 70.
Thamani ya sarafu ya nchi hiyo imeporomoka mara dufu na tayari kuna uhaba wa pesa katika miji mikubwa kama Khartoum.
Madaktari nao wamejitosa katika maandamano hayo leo Jumatatu ili kuongeza shinikizo dhidi ya Bashir shirika la habari la Associated Press limeripoti.
Bashir alichukua hatamu za uongozi katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwaka 1989.
Yapi yamejiri?
Maandamano ya Jumapili yalitokea wakati mamia ya watu wakitoka kutazama mechi ya mpira wa miguu.
Waifunga barabara na kisha kuanza kuimba nyimbo dhidi ya serikali kabla ya polisi kuwarushia mabomu ya machozi ili kuwatanya.
Awali, picha za video zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha maadamano hayo yaliendelea katika baadhi ya maeneo ya jiji.
Kamati Kuu ya Madaktari nchini Sudan imesema wanachama wake wamewapokea waandamanaji waliopata majeraha ya risasi na kuwa kuna watu kadha waliouawa.
Hakimiliki ya Picha @Shaimaakhalil@SHAIMAAKHALIL
Jumamosi mamlaka ziliwatia nguvuni viongozi 14 wa muungano wa upinzani wa National Consensus Forces akiwemo kiongozi wao Farouk Abu Issa mwenye umri wa miaka 85.
"Tunataka waachiwe huru mara moja, na kukamatwa kwao ni jaribio la dola kusimamisha harakati za mitaani," msemaji wa kundi hilo Sadiq Youssef amenukuliwa akisema.
Wapinzani wanasemaje?
Jumamosi, Sadiq al-Mahdi, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Umma, alipinga vikali "ukandamizwaji wa kijeshi" na kudai maandamano yamezalishwa na hali mbaya iliyoikumba nchi.
Pia ameitaka serikali ya Bashir kuachia madaraka kwa amani ama kukakabiliana na uma wa Wasudani.
"Itakuwa ni mpambano ambao serikali itashindwa, itaongeza makosa ya serikali na kuhitimisha muda wake," gazeti la Sudan Tribune lenye maskani yake Paris, Ufaransa limenkuu al-Mahdi akisema hivyo.
Polisi wakabiliana na wapenzi wa mpira wa miguu wanaompinga Omar al-Bashir
0
December 25, 2018
Tags