Rais Magufuli ataka kero za askari zishughulikiwe haraka

Rais Magufuli ataka kero za askari zishughulikiwe haraka
Rais John Magufuli amewataka viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani kushugulikia kero ndogo ndogo wanazokutana nazo askari katika mazingira yao ya kazi.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jana Desemba 21, 2018 katika hafla ya kuwatunuku vyeo maafisa na wakaguzi wasaidizi wa polisi iliyofanyika Kurasini Jijini Dar es salaam.

“Viongozi wa Wizara wa Mambo ya Ndani shughulikieni mambo madogo madogo, nimesikia wapo askari ambao wanahamishwa lakini hawalipwi fedha za uhamisho wakati kuna wengine wanalipwa,” alisema na kuongeza;

 “Kero ndogondogo zinawavunja moyo polisi, kwani wapo askari wanakamata wahalifu halafu wanapigiwa simu na ofisa wawaachie wakati wao wanatimiza wajibu wao,”

Rais Magufuli pia ameyataka majeshi yote ya polisi kushiriki katika shuguli za kiuchumi kwa kuanzisha viwanda ili waweze kujiendesha wenyewe.

“Ninataka muelekeo mpya wa majeshi yetu unaolenga kujenga uchumi wa kisasa, barabara nyingi kwa mfano kwenye Umoja wa Afrika zimejengwa na wanajeshi. Ninafahamu suala la sare za maaskari ni tatizo, ninataka nikiwaona askari wangu wawe wanapendeza hakuna ubaya kuwa na kiwanda kwani kitasaidia ninyi kujiendesha wenyewe,” alisisitiza Rais Magufuli

Aidha Rais Mgufuli amewapongeza wahitimu wote waliomaliza mafunzo na kuwasihi waendelee kuchapa kazi na kupambana na changamoto wanazokumbana nazo kwani haziwezi kuisha kwa siku moja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad