Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amesema kuna mzozo wa wazi kati ya taifa lake na taifa jirani na Rwanda katika kinachoonekana kuwa kudorora zaidi kwa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.
Rwanda na Burundi zimekuwa na uhasama kwa muda sasa, Burundi ikiituhumu Rwanda kwa kuhusika katika jaribio la kupindua serikali mwaka 2015 ambalo lilifeli.
Burundi hudai kwamba Rwanda iliwafadhili waliohusika na kwamba inatoa hifadhi kwao. Rwanda mara kwa mara imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.
Rais Nkurunziza amemwandikia barua mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Yoweri Museveni ambaye ni rais wa Uganda akisema Rwanda sasa si mshirika tena ndani ya jumuiya bali ni kama adui.
"Rwanda ndiyo nchi pekee katika kanda hii ambayo ndiyo moja wa wahusika wakuu katika kuvuruga uthabiti wa taifa langu na kwa hivyo siichukulii kama taifa mshirika, lakini kama adui ya nchi yangu," barua hiyo, ambayo inaonesha ilitiwa saini na Bw Nkurunziza tarehe 4 Desemba, imesema.
Kiongozi huyo anataka kufanyike mkutano maalum wa EAC wa kujadili mzozo huo kati ya Rwanda na Burundi.
Viongozi wa mataifa ya jumuiya hiyo ambayo kwa sasa inajumuisha Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na Sudan Kusini wamepangiwa kukutana tena 27 Desemba.
Hii ni baada ya mkutano wao wa karibuni zaidi kukosa kuendelea jijini Arusha kutokana na kutokuwepo kwa ujumbe kutoka Burundi.
Rais Pierre Nkurunziza asema Rwanda imekuwa adui, ataka kikao cha EAC kiandaliwe
0
December 08, 2018
Tags