RC: Wasafi waongeze ushirikiano na wasanii wa Zanzibar

RC: Wasafi waongeze ushirikiano na wasanii wa Zanzibar
WASANII wa Zanzibar na Tanzania bara wametakiwa kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina yao ili kusaidia maendeleo ya muziki wa kizazi kipya katika pande zote mbili za Jamhuri ya muungano Tanzania.

Wito huo umetolewa na mkuu wa mkoa wa mjini magharibi alipokutana na timu ya wasanii kutoka lebo ya 'Wasafi Clasic' ya Dar es salam na Zenji Flavour Unity (ZFU) ofisini kwake Vuga walipomtembelea kuelekea tamasha la Wasafi 2018 linalotarajiwa kufanyika kesho.

Ameeleza kuwa pamoja na kuwepo kwa mashirikiano ya muda mrefu, ipo haja pande mbili hizo kukaa chini na kufanya kazi pamoja ili kuimarisha vipaji vyao sambamba na kuwasaidia wengine kufiukia malengo yao.

Ayoub ambae pia ni mlezi wa chama cha wasanii wa muziki wa kizazi kipya Zanzibar alishauri kuanzishwa kwa mashindano ya kutafuta wasanii bora wa Zanzibar watakaoweza kuunganishwa na lebo ya muziki ya WCB rai ambayo iliungwa mkono na Afisa Mtendaji Mkuu wa lebo hiyo msanii Naseeb Abdul 'Diamond' na mlezi wa lebo hiyo Said Khamis Fela 'Mkubwa Fela.

Aidha Ayoub aliupongeza uongozi wa lebo hiyo na Mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar ZSSF kwa kukubaki kuwajumuisha wasanii wa Zanzibar katika tamasha hilo jambo alilosema litawasaidia kujitangaza na kuongeza uzoefu wa kushiriki matamasha makubwa kama hilo sambamba na kuwataka wazingatie sheria na taratibu zinazosimamia sanaa nchini.

Nae msanii Naseeb Abdul 'Diamond' amemshukuru Mkuu huyo wa mkoa kwa kuunga mkono kazi zinazofanywa na wasanii wa ndani na nje ya zanzibar jambo ambalo linawawezesha kuitikia kaulimbiu ya serikali zote mbili za kuwataka vijana kufanya kazi.

alisema, hatua ya serikali kuendelea kufuatilia shughuli zinazofanywa na wasanii zinathibitisha kuwaunga mkono ili wafikie ndoto zao jambo ambalo aliahidi kuliendeleza ili kundi kubwa zaidi linufaike.

Alieleza kuwa katika tamasha hilo mbali ya burudani wanayoitoa wameweza kufanya shughuli mbali mbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kutoa misaada katika taasisi za elimu, wajasiriamali na kwa Zanzibar wanategemea  kutoa misaada katika skuli na kituo cha afya cha Chumbuni ili viweze kutoa huduma nzuri kwa jamii.

Awali akitoa taarifa katika kikao hicho mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa ZSSF Khamis Thani alieleza kuwa mfuko huo umeamua kuungana na lebo hiyo ya muziki kwa lengo la kurudishga faida wanayoipata kwa jamii kwa kuimarisha wajasiriamali na kutoa misaada ya kijamii.

Tamasha la Wasafi linatarajiwa kufanyika kesho katika uwanja wa amani ambapo wasanii mbali mbali wa WCB na wa Zenji flavour wanatarajiwa kupanda jukwaani huku mkuu huyo wa mkoa akitoa ruhusa maalum ya kuendelea kwa tamasha hilo hadi saa 8 usiku.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad