Dar es Salaam. Mmiliki wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi ameeleza jinsi alivyokutana na mlimbwende wa Tanzania mwaka 2001, Jacqueline Ntuyabaliwe maarufu K-Lynn kwa mara ya kwanza jijini London, Uingereza mwaka 2010.
Akizungumza na kituo cha televisheni Citizen cha Kenya nyumbani kwake, Mengi amesema kama asingekuwa na mrembo huyo hadi sasa huenda angekuwa ameshafariki dunia.
Kinyume na watu wanavyofikiria anakiri kuwa haikuwa rahisi kumpata K-Lynn na huenda yeye ni miongoni mwa watu walionufaika na mashindano ya Miss Tanzania.
“Niliwahi kumsikia lakini hatukuwahi kuonana, lakini ikatokea nafasi wakati nipo safarini Uingereza ambako nilikuwa na shughuli za kibiashara na Jacqueline alikuwa yuko Jijini Birmingham kwenye shughuli zake za muziki.”
“Nilitaka kuonana naye wakati yupo Uingereza kwa hiyo nilimualika kuja London kutoka Birmingham, huwezi amini, hakuja!!! Lakini niliendelea kuwasiliana naye kwa simu mara kwa mara lakini hatukukutana. Tulipo rudi nyumbani Tanzania niliendelea kumfukuzia mpaka alipo kubali kwenda kwenye matembezi na mimi,” amesema.
Amesema baada ya kufunga ndoa na kupata watoto mapacha na mlimbwende huyo, Mengi mwenye miaka 75 anasema kwamba kama asingekuwa na mrembo huyo labda angekuwa ameshafariki.
Katika kitabu kinacholezea maisha yake ‘I can I must I will’, Mengi anamzungumzia mrembo huyo kama mtu aliye leta mwangaza katika maisha yake.
Tajiri huyo pia anazungumzia kwa nini anapenda kujihusisha na shughuli za kijamii pamoja na kujitolea kwa watu wasiojiweza.
“Mimi sijioni kama ni tajiri, bado najiona masikini kama wengine naamini kwamba kila kitu nilichonacho kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, kuna wakati watu wanajisahau na kufikiria kuwa yale walio nayo yametokana na nguvu au juhudi zao binafsi,” amesema Mengi akimueleza mtangazaji Jef Koinange.
“Jef hivi umewahi kufika katika msiba? Je, umewahi kumuona tajiri akichimba kaburi? Mwisho wa siku ni masikini ndio wanaochimba kaburi, matajiri mara nyingi hawapendi hata kuonyesha hisia zao. Nawapenda watu masikini maana huko ndiyo nilipotokea.”
Mwananchi