SIJUI ndiyo mgema akisifiwa tembo hulitia maji? Rose Muhando akiwa kwenye kilele cha umaarufu na mafanikio, akaanza kuwa miyeyusho. Akipewa pesa hatokei kwenye shoo. Maneno yakavuma kwamba Rose anagida sana kilevi na anabwia madude haramu.
Tatizo likawa Rose ana biashara kubwa. Shoo zake zinalipa. Shida siyo mwaminifu. Mapromota wa matamasha ya Gospo wakaanza kumkwepa. Maneno yakawepo kuwa Alex Msama ndiye pekee hummudu. Baadaye naye akachemka.
Hivi sasa Rose hana biashara tena. Thamani ya muziki wake ipo lakini watu wa kufanya naye kazi alishawatibua karibu wote. Hawamtaki tena. Aliyekuwa meneja wake tayari wameshakuwa maadui.
Amebaki kulalamika kuwa eti bora arudi kwenye dini yake ya zamani ya Uislam, kwamba katika Ukristo ananyanyaswa na kubaguliwa. Analaumu kuwa akilipwa pesa ya shoo, asipotokea anaitwa mwizi. Anajaribu kutetea tabia yake ya kula pesa za watu na kuingia mitini.
Rose amekuwa mtu wa kulalama na hakuna mwenye uthubutu wa kumsaidia. Wote wameshamchoka. Naye badala ya kupaona alipojikwaa, yeye yupo anapambana na mahali alipoangukia.
Rose ni kama Chidi Beenz. Fundi sana wa Hip Hop, ana nyota, swaga na mapafu ya kutosha jukwaani. Tatizo Chidi baada ya kulewa umaarufu akaamua kulewa mafanikio na madude haramu juu yake. Chidi akawa teja.
Chidi ameshapelekwa vituo vingi vya tiba ya kumwondoa kwenye uteja, kila akitoka anarudia madude. Wanamuziki wenzake, wamiliki wa vyombo vya habari, mapromota wa muziki, familia yake mpaka viongozi wa Serikali walishapambana weee kumsaidia Chidi lakini wapi!
Chidi naye hupenda sana kulaumu. Akiachwa bila kusaidiwa analaumu. Hivyo ndivyo Chidi na Rose wanafanana. Wana vipaji vikubwa na nyota, wana biashara na wanasaidiwa, ila wao hawataki kujisaidia. Matokeo yake wanazidi kuangamia. Chidi na Rose ni ubongo saresare.
Ndimi Luqman MALOTO