Polisi wanawake mkoa wa Arusha kupitia Mtandao wao (TPF NET) wamepongezwa kutokana na utendaji bora wa kazi zao za kila siku hasa katika suala zima la kudumisha nidhamu na kufanya kazi kwa uaminifu.
Pongezi hizo zimetolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ramadhani Ng’anzi wakati wa kuhitimisha maazimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili yaliyoanza rasmi Novemba, 25 mwaka huu.
Kamanda Ng’anzi alisema kwamba, askari wa kike wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wananchi lakini pia kudumisha nidhamu kwa kiwango cha hali ya juu katika utendaji wao wa kazi.
“Natoa pongezi kwa viongozi wenu wa TPF NET kwa kuwasimamia vyema na kuwaweka kwenye mstari mnyoofu na wale ambao walikuwa na dalili za kwenda kinyume na kazi walirudishwa kwenye njia kuu”. Alisema Kamanda Ng’anzi.
Alisema ubora wao wa utendaji kazi umekuwa kivutio kwa baadhi ya taasisi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali mkoani hapa ambapo wamekuwa wakifanya kazi pamoja nao hasa katika Madawati ya Kijinsia na Watoto kupitia harakati za kupinga ukatili na unyanyasaji na kuahidi kujenga ofisi kubwa ya Dawati mkoa itakayotoa nafasi ya faragha kwa wateja.
Akimkaribisha mgeni rasmi, kaimu Mwenyekiti wa Mtandao wa askari wanawake mkoani hapa, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Edith Makweli alisema kwamba, Mtandao huo kupitia Madawati hayo utaendelea kupambana ili kuweza kutokomeza vitendo vya ukatili na unyanyasaji.
Alisema kwa hivi sasa wameweka mipango inayolenga zaidi maeneo ya vijijini kwa wilaya za Arumeru, Longido na Ngorongoro ili wakatoe elimu ya madhara ya ukeketaji na ndoa za utotoni kwa jamii za vijiji husika.
“ Wakazi wengi wa mijini wana uelewa juu ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji aidha kwa kuhudhuria kwenye mikutano yetu au kupitia vyombo vya habari na kwa hivi sasa tumeamua kujikita vijijini tukaonane ana kwa ana na wanajamii na kwa nia ya kuwapa elimu sahihi. Alisisitiza Mrakibu huyo Msaidizi wa Polisi.
Naye Mkurugenzi wa CWCD (Center For Women and Children Development) Bi. Hindu Mbwego aliupongeza mtandao huo kupitia Dawati la Jinsia na Watoto kutokana na kuwa mstari wa mbele katika kutatua matatizo mbalimbali ya ukatili na unyanyasaji hali ambayo imetoa faraja kubwa baadhi ya wakazi wa mkoa huu ambao walikumbwa na matatizo.
Alilitaka Jeshi la Polisi liweke mikakati mipya ya kuwabana baadhi ya wana familia wanaovuruga ushahidi wa kesi za mimba za utotoni, ubakaji na ulawiti ili waweze kuchukuliwa hatua hali ambayo itasaidia kesi hizo kufikia mwisho na kuwa na matokeo chanya.
Wakati Mtandao huo wa Polisi wanawake ukitimiza miaka 11 toka uanzishwe Oktoba 25 2007 Jeshi la Polisi mkoani hapa liliitimisha maazimisho hayo ya kupinga ukatili kwa kuwafariji na kutoa zawadi ikiwemo Khanga kwa baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wodi mbalimbali za hospitali ya rufaa ya Mount Meru.
Picha no.1.Kaimu Mwenyekiti wa Mtandao wa askari wanawake (TPF NET) mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi Edith Makweli akikabidhi vifaa vya usafi kwa wafanyakazi wa hospitali ya rufaa ya Mount Meru wakati wa maazimisho ya siku 16 za kupinga ukatili yaliyofanyika mkoani hapa.
Picha no.2.Baadhi ya askari wa kike mkoa wa Arusha ambao ni wanachama wa TPF NET mkoa wa Arusha wakijiandaa kugawa Khanga kwa wagonjwa waliolazwa katika moja ya wodi wa wazazi iliyopo hospitali ya rufaa ya Mount Meru wakati wa maazimisho ya siku 16 za kupinga ukatili
Picha no.3.Kaimu Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi wanawake mkoani Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi Edith Makweli akimsalimia mtoto aliyelazwa katika hospitali ya rufaa ya Mount Meru pamoja na kumpa zawadi wakati wa maazimisho ya siku 16 za kupinga ukatili yaliyofanyika jana