Serikali Yawataka Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Kuwa Wazalendo

Serikali Yawataka Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Kuwa Wazalendo
Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi wametakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuwa wazalendo, wabunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Rai hiyo imetolewa leo na Jijini Dodoma na Naibu Wairi wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji wakati akifungua Kongamano la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi.

Amesema matokeo ya ukaguzi yanaonyesha kuwa kuna viashiria vya rushwa kwenye miradi ya umma, kitu ambacho kinatisha kwa maendeleo ya Taifa na hivyo kuwataka wataalaamu wa manunuzi na ugavi kuepuka vitendo hivyo viovu.

Dkt. Kijaji amesema kuwa program na miradi mingi ya Serikali haiwezi kufanyika bila kuhusisha ununuzi na ugavi na hivyo kuwataka wataalamu hao kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa ujuzi na weledi.

“Mafanikio yetu katika kuufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 yatatokana na umakini wetu, ubunifu wetu na uzalendo kwa Taifa letu,” alisema Dkt. Kijaji.

Aliongeza kuwa ubunifu ndio nguzo kuu ya mafanikio ya Taifa na kuongeza kuwa uzalendo wa hali ya juu utumike katika kusimamia mipango na miradi ya Serikali.

Aidha, Dkt. Kijaji amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imejipambanua katika kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo wataalamu wa ununuzi na ugavi hawana budi kutumia ujuzi wao kuhakikisha thamani ya fedha katika miradi yote inakuwa halisi.

Akisisitiza kuhusu ujenzi wa Tanzania ya viwanda, Dkt. Kijaji amesema kuwa viwanda vitachochea utoaji wa ajira, ongezeko la pato la Taifa na pato la mtu mmoja mmoja, hivyo kufanya maisha ya Watanzania kuwa bora.

“Viwanda vitaongeza uzalishaji na kufanya nchi yetu kuuza bidhaa nyingi nje ya nchi na kuongeza fedha za kigeni, na kwa mara ya kwanza tangu tupate uhuru Tanzania imekuwa na fedha ya kigeni ya kutosha kuagiza bidhaa toka nje kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kuwa ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki,” aliongeza Dkt. Kijaji.

Naibu Waziri Kijaji amesititiza suala ubunifu kutiliwa mkazo ikizingatiwa kuwa Tanzania kwa suala la ubunifu ipo chini ya ailimia 50, hivyo kuitaka Bodi ya Ununuzi na Ugavi kuwekeza zaidi katika ubunifu ili kufikia maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Sister, Dkt. Hellen Bandiho, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitatu imekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji elimu bure, kuboresha utoaji wa huduma za jamii kama vile afya na uwajibikaji kwa watumishi umma, kuboresha miundombinu na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ikiwemo ununuzi wa ndege unaoendana na ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Ameongeza kuwa hadi kufikia Desemba Mosi 2018, Bodi imesajili jumla ya wataalamu 10,863 katika ngazi mbalimbali za ununuzi na ugavi.

“Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi inatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli la kuhamia Dodoma na tumefanikiwa kupata ofisi za kupanga kwenye jingo la PSSSF, hivyo Bodi inatarajia kuhamia Dodoma hivi karibuni baada ya utaratibu wa kiutawala kukamilika,”alisema Dkt. Bandiho.

Hili ni Kongamano  tisa na linafanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma ambapo linahudhuriwa na washiriki kutoka mikoa yote ya Tanzania.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad