Shirika la Madini la Taifa (Stamico) lakabidhiwa Mtambo wa Kisasa Kuchoronga Miamba

Shirika la Madini la Taifa (Stamico) lakabidhiwa Mtambo wa Kisasa Kuchoronga Miamba
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, amelitaka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kutumia mtambo wa kuchoronga miamba kwa ufanisi ili kuliletea tija taifa.

Prof. Msanjila aliyasema hayo juzi wakati wa hafla fupi ya kuukabidhi rasmi mtambo huo kwa Stamico kwa ajili ya kuanza kuutumia rasmi.

Alisema ununuzi wa mtambo huo ni uwekezaji mkubwa ambao serikali imeufanya kwa Stamico, hivyo shirika hilo halina budi kuutumia vyema ili kuleta tija.

Kuhusu gharama za mtambo huo, Prof. Msanjila, alisema umegharimu Dola za Kimarekani milioni 1.3, ambazo akiwa mtendaji mkuu wa wizara anaona ni deni kubwa kwake, hivyo kuahidi kuusimamia ipasavyo ili kuhakikisha unazalisha faida na kuwa chachu ya kununua mitambo mingine kama hiyo ili kukuza sekta ya madini nchini.

Pia alilitaka shirika hilo kujitangaza vyema ili wananchi, hususan wadau wa madini wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji na utafutaji, kufahamu uwepo wa mtambo huo ili utumike hata kwa kampuni binafsi ili kujiongezea kipato na pia kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini.

“Kwa zabuni nilizozisikia mpaka sasa mtambo huu utazalisha pesa za kutosha,” alisema.

Prof. Msanjila pia aliitaka Stamico kuwasilisha taarifa za mapato na matumizi ya mtambo huo kila robo ya mwaka, ili kufanya tathmini endapo mtambo unatumika kwa faida.

Pia aliliagiza shirika hilo kuhakikisha mtambo huo unawezesha ununuzi wa mtambo mwingine mpya kila mwaka, ili ndani ya miaka mitano shirika limiliki mitambo mitano na kurahisisha utekelezaji wa shughuli za uchimbaji na utafutaji wa madini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad