Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeeleza masikitiko yake kutokana na tuhuma zilizotolewa na mteja na mteja wao ambaye pia ni msanii maarufu wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz mkoani Mwanza kupitia video iliyosambaa kwenye mitandao wa kijamii akidai kuwepo kwa huduma mbovu kwa baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo.
Akizungumza na wanahabri leo, Msemaji wa ATCL, Josephat Kagirwa amesema tuhuma zilizotolewa na Diamond kuwa limeuza tiketi yake baada ya kubaini kuwa alichelewa kufika uwanjani siyo za kweli, na kwamba mteja huyo ameomba kusafiri tarehe inayofuata (leo).
“Diamond alishindwa kusafiri na ndege ya shirika yetu kutoka Mwanza kwenda Dar jana, kwa sababu alichelewa kufika uwanja wa ndege na tiketi yake haikuuzwa kwa mtu mwingine, bali ataitumia leo jioni. Hivi sasa tumezidi kujiimarisha, tunaruka katika viwanja 11 hapa nchini , na tunaruka viwanja vingine 3 vya nje ya nchi,” amesema Kagirwa.
Jana, Diamond aliwatolea uvivu wafanyakazi wa Air Tanzania Tawi la Mwanza akidai kuwa amekuta tiketi zake alizokuwa amezifanyia Booking zimeuzwa kwa watu wengine na kuelezwa kuwa hawezi kuondoka na ndege kwa kuwa alikuwa amechelewa, lakini muda mfupi baada ya yeye kuzuwiliwa kuingia eneo la watu wanaosafiri Diamond alisikika akisema “kwanini huyo ameruhusiwa kuingia kwani yeye hajachelewa?”