Simbachawene Amchapa Makofi Dereva wa Lori

Simbachawene Adaiwa Kumchapa Makofi Dereva wa Lori
Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), George Simbachawene anadaiwa kumchapa makofi na kumjeruhi, Kassim Abdalla Kassim kwa kosa la kuegesha lori lake karibu na Prado ya Mbunge huyo wa Kibakwe.

Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kutokea Desemba 24 mwaka huu, usiku wa Mkesha wa Sikukuu ya Krismasi katika baa ya Titanic iliyoko Vingunguti, jijijini Dar es Salaam ambayo inamilikiwa na Waziri huyo wa zamani wa Serikali ya awamu ya nne na tano.

Kutokana na tukio hilo, Simbachawene ambaye kwa sasa ni
Mbunge wa Kibakwe na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Bajeti, amehojiwa katika Kituo cha Polisi Buguruni, akituhumiwa kushirikiana na vijana wake kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili Kassim na kusababisha alazwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Simbachawene anadaiwa kumshambulia kijana huyo kwa kushirikiana na vijana wake wakiwemo walinzi wa baa hiyo ya Titanic.

Alipotafutwa Simbachawene alisema kuwa dereva huyo wa lori alipigwa na watu wa bodaboda na wateja waliokuwa kwenye baa yake baada ya kuingiza lori lake vibaya.

“Unajua pale Titanic kuna yard ya magari ya kampuni ya huyo dereva. Sasa sehemu ile ni ndogo yeye aliingiza gari kwa nguvu na kuibua taharuki, kweli watu walimfuata, wakampiga lakini mimi sikuhusika sasa naona wanajaribu kutengeneza picha ya kuchafuana,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa ukisha kuwa kiongozi, baya lako nzuri lako.

Hata hivyo taarifa zinasema kuwa siku ya tukio inadaiwa kuwa Kassim alifika katika baa hiyo iliyo jirani na ofisi yao kwa ajili ya kuegesha gari lake, lakini ghafla alishangaa kuona anapokea kichapo kutoka kwa walinzi.

Akizungumza kwa shida akiwa kitandani katika Wodi ya Sewahaji namba 18, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Kassim alisema siku hiyo alikuwa akirejea kutoka nchini Burundi na kwamba alikwenda katika baa hiyo kwa ajili ya kuegesha gari alilokuwa akiendesha namba T 334 AUX Scania.

Alisema alipitisha gari lake kando ya lilipoegeshwa Prado, mali ya Simbachawene bila hata kuligusa lakini alishangaa kuona meneja wa baa hiyo inayodaiwa kumilikiwa na mbunge huyo wa Kibakwe, Brayson Mulungu alimfuata na kuanza kumshutumu kwa nini ameliziba gari la Mheshimiwa.

“Wakati tunazungumza na Meneja, Simbachawene alikuja na kunipiga kibao.

Baadaye aliwaamuru walinzi wa baa hiyo wanipige, nikapigwa, nikaumia sehemu mbalimbali za mwili.

“Tulikimbia kituo cha Polisi Buguruni kwa ajili ya kutoa taarifa
tukafanikiwa kupata RB baada ya hapo nikapoteza fahamu nilipozinduka nilijikuta nipo Muhimbili,” alisema.

Inadaiwa kuwa tayari Simbachawene amefika kituo cha Polisi buguruni ilikofunguliwa RB namba 11587/2018 ya shambulio
la kudhuru mwili ambapo amehojiwa na suala hilo hivi sasa linaendelea na uchunguzi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad