Siri nzito Wachaga kutoingiza maiti usiku


Moshi. Ni kawaida kwa makabila mengi nchini kuzika miili ya wapendwa wao katika mikoa au maeneo ya asili ya ukoo au familia husika.

Ndio maana baadhi ya watu wanapofariki dunia husafirishwa na kupelekwa kuzikwa katika mikoa yao ya asili.

Moja ya makabila yenye utamaduni huo ni Wachanga kutoka katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Wachaga wana mila nyingine zaidi kwani wanaposafirisha mwili wa marehemu kwenda kuuzika kijijni huwa hawaendi moja kwa moja nyumbani na hasa inapofika jioni au usiku, mwili hutakiwa kufika kijijini alfajiri, hivyo msafara huweka ‘kituo’ mahali kusubiri mpaka kunapokucha.

Mara nyingi kambi hiyo huwekwa katika baa au maeneo mengine ya karibu na kijiji wanachokwenda.

Hilo limekuwa likiibua maswali kwa watu wengi miongoni mwao wakiona kuwa huenda mila na desturi za kabila hilo zinakataza kuingiza maiti ndani usiku.

Mwananchi limepita maeneo mbalimbali mjini hapa kudodosa ili kupata ukweli kuhusiana na suala hilo.

Louis Mbuya, mkazi wa Kilema mjini Moshi anasema watu kupumzika mbali kidogo na nyumbani kwa marehemu ni utaratibu tu ambao wamejiwekea.

Anasema si vizuri kuingia nyumbani usiku na mwili wa marehemu wakati watu wamelala kwa kuwa wataamka na kuanza kulia au kupiga kelele.

“Kunapotokea msiba na watu wanajua kwamba maiti inatoka mbali kuletwa nyumbani, huwa inasafirishwa na wakifika karibu na nyumbani usiku hawawezi kuipeleka mpaka kuche,” anasema.

“Hakuna sababu za kimila katika hilo, hapa ni kwamba wanahofia kuamsha watu usiku kupokea maiti kwa sababu kawaida ni lazima watu walie na kupiga kelele, hivyo si vizuri kuamshwa usiku.”

Fanuel Silayo anasema utaratibu huo unatoa fursa kwa wanafamilia kujiandaa kuupokea mwili wa marehemu na ni kama heshima kwa mtu waliyempoteza.

Anasema, “Usiku watu wamelala, si vizuri kupeleka mwili na hili ni kama heshima za kuupokea mwili badala ya kuingia kimyakimya watu wakiwa wamelala.”

Silayo anasema: “Unapoona watu wamepumzika baa, hotelini au mahali pengine karibu na nyumbani kusubiri kupambazuke wanawaachia wanafamilia na waombolezaji wengine kujiandaa kwa heshima ya kuupokea msafara wenye mwili wa marehemu.”

Naye Stewart Lyatuu anaeleza kuwa, “Naomba muelewe kuwa si suala la mila, ni utaratibu na hili ni kwa sababu ya watu kupumzika na kupata chochote kwa kuwa kama mnavyofahamu maiti ikiingia nyumbani kunaibuka kelele na watu wengine hushindwa kula kutokana na majonzi ”

Agness Mushi, mkazi wa Uru, anasema tangu alipozaliwa miaka zaidi ya 60 iliyopita amekuta utaratibu huo na amekuwa akisikia kwamba wanaosafirisha maiti huwasubiri watu nyumbani wajiandae kabla ya kuwasili.

“Ni kweli wakileta maiti lazima wasubiri mahali, lakini sijui kama kuna sababu za kimila,” anasema.

“Jambo jingine ambalo nimeliona pia ni kwamba kama kaburi limeshachimbwa halafu maiti ikachelewa kuzikwa siku hiyo, lile kaburi haliachwi, yaani wachimbaji watabaki huko kuendelea kuchimbachimba hata na kijembe kidogo hadi maiti ifike.”

Anasema wachimbaji wanaweza kukesha katika eneo la kaburi wanachimbachimba.

“(Hii hutokea) wakati mwingine watu wanaweza kuwa wanasafirisha maiti halafu ikatokea ajali wakashindwa kufika, hivyo wachimbaji huwa wanabaki kule kuonyesha kazi ya uchimbaji inaendelea mpaka maiti itakapofika nyumbani.”

Wakati hao wakisema huo ni utaratibu wa kawaida, Profesa John Boshe, mkazi wa Kibosho, anasema suala hilo linatafsiriwa kwa namna mbili wakiwapo wanaodai kuhofia taharuki na wengine imani na kuogopa mikosi.

Anasema wanaoogopa kufikisha maiti nyumbani mapema huhofia kuibua taharuki na kelele.

“Kumfikisha marehemu mapema nyumbani kunaweza kuleta taharuki kwa wafiwa na majirani kuanza kuomboleza mapema na kupiga kelele, haipendezi,” anasema Profesa Boshe.

Jambo la pili, anasema, ni imani na mila, kwamba mwili wa marehemu ukifikishwa unatakiwa kwenda kuzikwa moja kwa moja.

Anasema pia wapo wanaoamini kwamba mwili wa marehemu ukiwekwa ndani unaweza ‘kumvuta’ mtu mwingine akafa, na imani hiyo iko kwa baadhi ya watu na si Wachaga wote.

“Hii ndiyo maana kaburi huandaliwa siku hiyo mapema na maiti ikifikishwa nyumbani huingizwa kwenye nyumba anayotakiwa kuingizwa na akitolewa anapelekwa kaburini.”

Hata hivyo, Silvester Temba anasema hakuna sababu za kuendelea na imani hiyo kwa vile haina madhara kwa wafiwa au watu wengine.

“Sioni sababu ya kuendelea kuamini mila zilizopitwa na wakati kwa kuwa toka tumezaliwa tunaona hayo yanatendeka, lakini hatujawahi kushuhudia madhara kwa watu ambao wamekuwa hawaamini mila hizo,” anasema.

Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad