SSRA Yawatoa Hofu Wastaafu......Yaendelea Kupokea Maoni Kuhusu Mafao

SSRA Yawatoa Hofu Wastaafu......Yaendelea Kupokea Maoni Kuhusu Mafao
Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA) inaendelea kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau na wananchi ambayo yatasaidia kuboresha kanuni na miongozo itakayoendelea kumnufaisha zaidi mstaafu kupitia mafao yake.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Dk. Irene Isaka, alisema lengo la mamlaka hiyo ni kuendelea na maboresho ya kanuni na miongozo, kwani dirisha la maoni lipo wazi kwa watanzania kuleta mawazo yao yatakayosaidia
kuboresha mfumo wa mafao kwa wastaafu.

“Milango ipo wazi kwa wananchi na wadau mbalimbali kuleta maoni yao, ili tuboreshe sheria na kanuni zinazoongoza mifuko ya jamii na kuongeza tija katika mafao ya wastaafu,’’ alisema Dk. Isaka.

Alieleza kuwa kanuni zinazotumika sasa zimetokana na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyakazi, waajiri na kwa ujumla katika kutoa maoni na mapendekezo yamesaidia kupatikana kwa sheria na kanuni ambazo zimeleta neema kwa wastaafu kwa kupata mafao stahiki na kwa wakati.

“Taratibu za mafao zinampa mstaafu nafasi ya kupata mkopo
katika baadhi ya benki nchini kutokana na uhakika wa pensheni yake kwa kipindi cha kustaafu kwake na kumfanya aweze kuendelea kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema.

Dk.Isaka alisema tofauti na miaka ya nyuma pensheni za wastaafu zilikuwa na ukomo wa muda wa miaka 10 mpaka miaka 12, lakini kwa kanuni za sasa pensheni ya mstaafu atapokea kwa kipindi chote cha maisha yake ya kustaafu, hii inampa uhakika wa kupata mkopo na kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Moja ya majukumu ya SSRA ni kulinda na kutetea maslahi ya mwanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii hivyo tutaendelea kupokea maoni ili mwanachama anufaike zaidi kupitia michango yake atakapostaafu,” alisema.

Alisema SSRA itaendelea kuwaelimisha wanachama na wananchi kwa ujumla juu ya kanuni mpya ya ukokotoaji na faida zake kwa wanachama pale atakapo staafu, kwani imeonekana uelewa wa hii kanuni mpya haijawafikia watu wengi nchini na hata wale wachache waliofikiwa na taarifa hiyo wengi wao wamepotoshwa.

“SSRA tumejipanga kuwafikia wanachama wote nchini na
kuwapa elimu juu ya kanuni hii mpya ya ukokotoaji wa mafao ili kuwaondoa katika hofu ambayo imejengeka miongoni mwao kutokana na maneno ya baadhi ya watu wasio na uelewa wa kutosha juu ya kanuni mpya ya Ukokotoaji mafao,” alisema Dkt. Isaka.

Alisema madhumuni ya mamlaka hiyo ni kumuondoa mstaafu katika hali mbaya ya kiuchumi baada ya kumaliza mafao yake ya mkupuo ya asilimia 25, kwa kumpatia asilimia zilizobaki kama pensheni ya kila mwezi kwa kipindi chote cha maisha yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad