Sumatra Yaruhusu Magari Madogo Kusafirisha Abiria Mikoani

Sumatra Yaruhusu Magari Madogo Kusafirisha Abiria Mikoani
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesema imepanga kusajili magari zaidi, yakiwamo mabasi madogo, kwa ajili kusafirisha abiria katika kipindi chote cha mwisho wa mwaka.


Akizungumza na Nipashe juzi, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johanes Kahatano, alisema lengo ni kuhakikisha wanatatua changamoto ya usafiri na adha ambayo wananchi huipata katika kipindi cha mwisho wa mwaka.
Alisema magari yatakayosajiliwa ni yenye ubora na yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 30.


“Ni kweli tumeamua kuongeza magari kwa kusajili magari mengine ya muda yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 30 kwenda juu, ambayo tutakuwa tumejiridhisha kuwa yana ubora huo wa kusafirisha abiria," alisema Kahatano na kueleza zaidi;


"Lakini tutahakikisha kwamba madereva wote wenye magari hayo wanazingatia sheria na tutahakikisha kwamba yote yamefungwa vidhibiti mwendo kwa ajili ya usalama kwa abiria na yeyote atakayekiuka sheria atachukuliwa hatua kali."
Alisema wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na idadi kubwa ya wananchi ambao hupendelea kusafiri kwenda sehemu mbalimbali za nchi kwenda wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka.


Mbali na kufunga vidhibiti mwendo, mkurugenzi huyo aliyataja masharti mengine ambayo wameyatoa kwa wafanyabiashara wenye magari madogo ya abiria ni kuhakikisha wanazingatia viwango vya nauli.


Alisema mamlaka itayakagua kwanza magari hayo kujiridhisha kuhusu ubora na usalama wake kabla ya wamiliki wake kupewa kibali cha kusafirisha abiria kwenda mikoani.


“Katika kudhibiti uongezaji holela wa nauli, tumejipanga vya kutosha na tutahakikisha hakuna dereva anayeongeza nauli kiholela, na timu za usimamizi zitakuwapo kila mahali,”alisema Kahatano.
“Pia tumetoa namba maalum ambayo abiria watakuwa wanaitumia kuuliza viwango vya nauli kupitia simu zao za mkononi kutoka mkoa wanapotoka hadi wanapoelekea.


"Kwa hiyo, wasikubali kuibiwa, kiwango chochote cha nauli  mahali popote unapoenda ukiuliza Sumatra kupitia mfumo uliowekwa unapata majibu na wiki hii tunaanza kutoa elimu hiyo.
"Kadri idadi ya abiria itakavyokuwa ikiongezeka, ndivyo na sisi tutavyokuwa tunaongeza kusajili magari."


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad