Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini Tanzania TFF kupitia kwa Mwenyekiti wake, Ally Mchungahela imekataa ombi la Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ambayo iliomba kuahirishwa kwa usaili wa wagombea na badala yake zoezi la uchukuaji fomu kuanza upya.
Alhamisi ya Disemba 6 ndiyo ilikuwa siku ya usaili wa wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya klabu ya Yanga, ambapo viongozi wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga walileta ombi la kutaka kuahirishwa kwa zoezi hilo na kuanza mchakato wa uchukuaji fomu utakaosimamiwa na klabu, ombi ambalo liliibua sintofahamu katika zoezi hilo la usaili.
Akizungumza kuhusiana na sintofahamu iliyotokea katika zoezi hio la usaili, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Ally Mchungahela amesema,
"Awali tulikubaliana mkutano uanze saa nne, mwakilishi wao amefika hapa saa nane halafu amekuja na vitu vipya kabisa tofauti na tulivyokusudia kujadili".
"Kwa nafasi yangu nikiwa kama Mwenyekiti, sijakubaliana na hoja hiyo. Tutaendelea na zoezi letu la usaili kama kawaida na uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa," ameongeza Mchungahela.
Wagombea ambao walifanyiwa usaili ni pamoja na wagombea wa nafasi ya Uenyekiti na Makamu Mwenyekiti huku zoezi hili likitarajiwa kuendelea tena leo kwa wagombea wa nafasi ya Ujumbe.