Tundu Lissu Akubali Kugombea Urais 2020 Kama Atapitishwa na Chama Chake

Tundu Lissu Akubali Kugombea Urais 2020 Kama Atapitishwa na Chama Chake
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema yupo tayari kugombea urais ikiwa vyama vya upinzani vitampa ridhaa hiyo.

Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7 mwaka jana akiwa Dodoma na watu wasiojulikana, amesema hayo jana katika mahojiano na na gazeti la Mwananchi

Mwanasiasa huyo alisema yeye ni mwanachama wa Chadema na hawezi kufanya jambo pasi na kuridhiwa na chama chake au vyama washirika wa Chadema kwani kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu na maadili.

Kauli ya Lissu kuhusu kugombea urais mwaka 2020 imetokana na swali aliloulizwa kutokana na kuwa miongoni mwa wanasiasa wa upinzani wanaotajwatajwa, “Wakikaa katika vikao na kunipa bendera, nitakubali kubeba msalaba huo mzito kwa mikono miwili.”

Pia aliulizwa, ikiwa hataombwa na chama atajitosa mwenyewe kuwania nafasi hiyo? Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alisema, “Maadili yangu, unaambiwa ukiwa katika chama lazima upewe fursa kwa hiyo nitasubiri fursa hiyo.”

Kuhusu afya yake, Lissu ambaye ni mnadhimu mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni alisema anatarajia kuanza mwaka akiwa hana vyuma alivyowekewa Julai 9 katika mguu wake wa kulia ili kuunganisha mifupa.

“Desemba 31 nitafanyiwa upasuaji wa mwisho wa kuondoa hii antena ambayo nimekaa nayo kwa miezi sita tangu Julai 9 na nimeelezwa na madaktari kuwa mfupa uliokuwa uunge umeunga na mfupa uliotakiwa kuota unaendelea vizuri,” alisema Lissu na kuongeza:

“Yaani Jumatatu (Desemba 31) nitahitimisha kazi ya kitabibu na nitaanza mwaka mpya (2019) na mguu mpya ambao hauna chuma.”

Lissu alisema baada ya kuondolewa kwa vyuma, kitakachofuata ni mazoezi ya kutembea na taratibu ataachana na magongo.

Baada ya hapo, Lissu alisema ataanza kuhudhuria vikao mbalimbali ambayo amealikwa katika mataifa ya Ulaya.

Alisema Januari 14 amealikwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na Umoja wa Ulaya (EU) Brussels, Ubelgiji na Februari mwakani amepata mwaliko wa wiki moja huko Washington Marekani.

“Huko kote nakwenda kuzungumzia kile kilichonitokea Septemba 7 (mwaka jana) lakini kile ambacho kinaendelea nyumbani (Tanzania) na mambo mengine,” alisema.

Alipoulizwa kwamba kuanza wake kusafiri nchi mbalimbali bila shaka ni wakati wake wa kurejea nyumbani, mwanasheria mkuu huyo wa Chadema alisema, “Katikati ya mwakani naweza kurejea. Kuanza mazoezi hakutanizuia kurejea kwani naweza kurudi nyumbani na nikawa nakuja huku (Ubelgiji) kwa madaktari.”

Hata hivyo, Lissu alisema hilo la kurejea nchini litafanikiwa baada ya kufanya mazungumzo na watu mbalimbali ikiwamo viongozi wenzake wa kisiasa pamoja na Serikali.

“Serikali itapaswa kunieleza usalama wangu utakuwaje baada ya kurejea, ingawa jukumu la Serikali ni kulinda raia wake na mimi ni miongoni mwao hasa ukizingatia kile kilichonitokea,” alisema.

Akigusia harakati zake za kupigania demokrasia, Lissu alisema , “Kama nilivyowahi kusema, sitarudi nyuma na mapambano ya kupigania demokrasia si ya wanasiasa pekee, bali makundi mbalimbali kama madaktari, waandishi wa habari, wakulima, wavuvi, bodaboda na wengine.”

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Jamani kweli mmekosa Dili NI magoigoi na Viwete.
    Hatukupeni nchi...!!!
    HIVYO HATA HAYA HAMNA..!!!

    TUNATAKA JEMBE CHAPA YA SIMBA AU NYATI.. MNALO?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad