Kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema kuwa anashangazwa na uwezo wa wachezaji wake wakiwa uwanjani hali ambayo ilimfanya ashindwe kuzungumza na kutokwa na machozi kutokana na hisia kali baada ya mchezo wa juzi dhidi ya Tanzania Prisons ambao walishinda bao 3-1.
Yanga walicheza mchezo wao wa 14 na kufanikiwa kuendeleza rekodi ya ushindi kwa mechi zote tatu za mkoani ambazo wamezicheza hali ambayo imewafanya wazidi kuwa kileleni kwa kujikusanyia pointi 38 wakiwa wameshinda jumla ya michezo 12.
Zahera amesema anashangazwa na uwezo wa wachezaji hasa wakiwa uwanjani kwa namna wanavyopambana kutafuta matokeo ambayo ni zawadi kwa mashabiki.
"Hisia kali zilinitawala baada ya mchezo kwa kuwa kuna mengi ambayo wachezaji wangu wanapitia inanishangaza kwa kuwa wanapata matokeo katika mazingira ambayo hutarajii kabisa hali ambayo inanifanya nidhani nina deni kwao.
"Mashabiki wanafurahia kupata ushindi hilo ni jambo jema ila wanapaswa watambue kuwa wachezaji wangu wanacheza kwa kujitolea hivyo ninafurahi kuona wanafurahi," alisema.
Kocha Zahera baada ya mchezo alishindwa kueleza sababu ya kuweza kufanya mabadiliko yaliyoleta matokeo mazuri hali ambayo ilimfanya atokwe na machozi wakati alipokuwa akihojiwa na mtangazaji wa kituo cha Azam Tv.