Wafanyakazi 93 wa kampuni ya madini ya Acacia wamehitimu mafunzo maalum ya uongozi ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza na waandishi wa habari Janeth Reuben, Meneja Mkuu wa Uboreshaji Tija, alisema mpango wa mafunzo ulianzishwa mwaka 2016, wakati nchi ikiendelea na mapinduzi ya viwanda.
Alisema wahitimu wa mpango huo wapo katika nafasi nzuri ya kuchangia katika ukuaji wa sekta ya madini nchini.
Aliongeza lengo kubwa ni kuwapa elimu wazawa na kupunguza wimbi la wageni ambapo kwa programu mbalimbali zinazoendeshwa na Acacia zimewezesha kampuni hiyo kupunguza utegemezi kwa wafanyakazi wa kigeni kwa asilimia 85 ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita hadi kufikia mwaka jana, asilimia 96.2 ya wafanyakazi wa Acacia walikuwa Watanzania.
Alisema mipango yote ya mafunzo ya kitaaluma inayotolewa na kampuni hiyo hutoa jukwaa muhimu kwa wafanyakazi wazawa kushika nyadhifa za uongozi pamoja na kushiriki katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kusaidia mapinduzi ya viwanda.
"Mpaka sasa ni jumla ya wafanyakazi 297 walihitimu mpango huu wa Rainbow kutoka migodi mitatu ambayo ni Acacia, North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake tunawathamini sana wafanyakazi wetu, hivyo tutaendelea kutoa elimu zaidi,” alisema Reuben.
Baadhi ya wahitimu Frenk Ngoroma na Annastazia Mbunda, walisema mwanzo hawakuwa na uwezo mkubwa wa kupangilia kazi kusimamia wenzao, hivyo ujuzi walioupata kutoka katika mafunzo hayo vitawawezesha kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na kuupeleka ujuzi huo hata nje ya kampuni.
“Mwanzo nilikuwa napata changamoto sana, hasa kipindi walipokuwa wanakuja wageni kwa sababu walikuwa wanakuja na vitu vyao ambavyo ni vigeni vilinipasa nijifunze, lakini nilipopata mafunzo hayo ya kuwa kiongozi bora nimejifunza mbinu mbalimbali na nina ujuzi wa kutosha wa kuwa kiongozi bora,” alisema Mbunda.
Wafanyakazi wa Kampuni ya Acacia Wapewa Mafunzo Maalum
0
December 11, 2018
Tags