Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakurugenzi kutosheherekea sikukuu ya Christmas mpaka watakapopata ufumbuzi wa ujenzi wa madarasa 99 yanayohitajika kwaajili ya kutumiwa na wanafunzi 4930 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka 2019.
Ametoa maagizo hayo wakati akitoa salamu zake za Christmas kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa ambapo amesema kuwa ufaulu mwaka huu 2018 umekuwa kwa asilimia 73 ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo ulikuwa ni wa asilimia 68 na hivyo wanafunzi 4930 kukosa kuingia madarasani kutokana na changamoto ya upungufu wa madarasa.
Ameongeza kuwa serikali ya Mkoa imejipanga vilivyo kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayekosa nafasi ya kusoma hali ambayo itawafanya wanafunzi wote waliokosa nafasi kupatiwa fursa ya kuendelea na masomo yao kwa mwaka 2019.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewaomba wanachi kwa kushirikiana na halmashauri kuhakikisha vyumba hivyo vinapatikana hadi kufikia mwishoni mwa mwezi wa pili.
“Hawa wanafunzi tusiwakatishe tamaa ya kukosa nafasi ya kwenda kidato cha kwanza, hakuna mwanafunzi hata mmoja ataacha kwenda kidato cha kwanza, wakuu wa wilaya wote wasimamie zoezi hili na hakuna likizo na wale wakurugenzi wote hakuna kwenda likizo mpaka vyumba vya madarasa vyote view vimekamilika,” amesema.
Kati ya hayo madarasa 99, halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga inatakiwa kujenga madarasa 41 yatakayotumiwa na wanafunzi 2,042, huku Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ikihitaji madarasa 27 ili kutumiwa na wanafunzi 1,365.
Halmashauri zingine ni Wilaya ya Nkasi inayohitajika kujenga madarasa 19 kwaajili ya wanafunzi 925 na halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ikitakiwa kujenga madarasa 12 kwaajili ya wananfunzi 598.