Waliowapa mimba wanafunzi 16 watangaziwa kiama

Waliowapa mimba wanafunzi 16 watangaziwa kiama
Wakuu wa wilaya katika mkoa wa Pwani wameagizwa kuhakikisha wanawapa misukosuko na kuwakamata waliohusika kuwapa mimba wanafunzi 16 na kusababisha kushindwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo na kusema kuwa  serikali haiwezi kuvumilia watu hao waendelee kutamba mitaani wakati wameharibu maisha ya wasichana wadogo, huku akiwataka wazazi na walezi kuacha kumaliza kesi za mimba za utotoni majumbani.

Alisema wazazi kwa kiasi wanachangia watoto wao kuharibika kwa kuwa wamekuwa tayari kurubuniwa kwa fedha ili kuwaachia huru wanaobainika kuwapa mimba watoto wao wa kike.

Kuhusu kushuka kwa ufaulu Ndikilo alisema wanafunzi 223 ambao ni sawa na asilimia 0.74 hawakufanya mtihani wa kumaliza darasa la saba, kutokana na utoro 149,mimba 16 ,ugonjwa 15,vifo tisa na sababu nyingine 34.

Alitaja tatizo jingine kuwa ni utoro,mdondoko suala ambalo linachangia kushusha taaluma.

“Tuna kazi ya ziada kukabiliana na mdondoko mashuleni, tunalea watoto kuacha shule, wilayani Mkuranga mdondoko ulikuwa 67,Kibiti 36,Chalinze 36,”

“Kisarawe wanne, Bagamoyo 12,Mafia wanne, Kibaha Mjini tisa na Kibaha Vijijini wanne “alifafanua Ndikilo.

Awali katibu tawala mkoani hapo, Theresia Mbando alieleza, idadi ya wahitimu waliosajiliwa kufanya mtihani ,walikuwa 30,010 kati yao wavulana 14,304 na wasichana 15,706 ambapo waliofanya mtihani huo ni watahiniwa 29,787 wakiwemo wavulana 14,182 na wasichana 15,605 sawa na asilimia 99.26.

Ofisa elimu mkoa Abdul Maulid alisema, halmashauri ya Chalinze waliopata mimba ni Tisa, Mkuranga wanne ,Bagamoyo mmoja, Kisarawe mmoja na Rufiji mmoja.

Alieleza kuwa licha ya hali hiyi matokeo yanaonyesha kupanda kwa ufaulu kimkoa kutoka asilimia 66.9 mwaka jana hadi asilimia 77.79 mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad