Wambula Atoa ya Moyoni Apania Kufika FIFA

Wambula Atoa ya Moyoni Apania Kufika FIFABaada ya Mahakama Kuu kumrejesha kwenye nafasi yake Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Novemba 30, Michael Richard Wambura, leo Jumanne ametinga katika ofisi za shirikisho hilo akisema amerejea rasmi baada ya kukaa nje kwa takribani miezi tisa tangu alivyofungiwa mwanzoni mwa mwaka huu kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa fedha.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Kamati ya Maadili ya TFF  ilitangaza kumfungia Wambura maisha kutojihusisha na soka kutokana na kukutwa na makosa matatu, ikiwemo kuchukua fedha za TFF ambazo ni za malipo ambayo  hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.

Pili ni kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya Kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo siyo halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.

Na Tatu, ni kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho hilo ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF kama ilivyorekebishwa mwaka 2015.

  Wambura amesema amewasilisha Shauri la Mahakama Kuu  TFF baada ya kutengua maamuzi ya Kamati ya Maadili ya TFF ambayo ilimfungia maisha kujihusisha na soka kutokana na makosa hayo matatu, hivyo anachosubiri hivi sasa ni utendaji kutoka TFF.

“Nimefikisha shauri la Mahakama Kuu juu ya kutengua maamuzi ya Kamati ya Maadili ya TFF ambayo ilinifungia maisha iliyotolewa tangu Novemba 30, mwaka huu, mimi ni makamu wa rais wa TFF, hivyo nimekuja kuwakabidhi ili utekelezaji uanze mara moja, nimeleta ili wasije kusema hawakupata taarifa.

“Imekuwa ikizungumzwa kuhusu kupeleka masuala ya mpira mahakamani, kilichokwenda kuzungumzwa ni suala la uvunjifu wa sheria uliofanywa na Kamati ya Maadili ya TFF na si kupeleka masuala ya mpira mahakamani, kabla sijalipeleka shauri hili mahakama kuu, niliwaandikia barua TFF tarehe 16 mwezi wa nne kuomba kulimaliza suala hilo kabla ya kufika huko, walikaa kimya.

“Nilifungua shauri hili mahakamani tarehe 29 mwezi wa tano, ikiwa ni chombo cha mwisho  kinachotoa haki ili kutoa maamuzi, na TFF walikuwa wakihudhuria katika shauri hilo mwanzo hadi mwisho.

“Wanachotakiwa kufanya TFF kwa sasa ni kufuata njia mbili aidha kukubaliana na maamuzi ya mahakama ama kukata rufaa na iwapo watakaa kimya kabisa watakuwa wamedharau mahakama na itakuwa chombo cha kwanza kuidharau mahakama na iwapo haijatekelezeka basi njia bora itakuwa kulipeleka suala hili kwenye chombo husika ambapo ni FIFA ili waweze kuja na kuona nini kinaendelea nchini kwetu.

“Natarajia kukutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe ambaye ndiye msimamizi wa michezo nchini ili tuweze kumueleza na aweze kutusaidia kwa upande wa serikali.

“Maajabu ni kwamba kwa mara ya kwanza imetokea Tanzania kuweza kufungia viongozi watatu wa Kamati ya Utendaji ndani ya miezi sita, ndiyo maana wakati viongozi wa FIFA walipokuja nchini kule Dodoma tulipofanya uchaguzi  walituambia kuwa tuna matatizo ya suala la katiba na hili linaonekana wazi linatakiwa ufumbuzi.” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad