Aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura, kabla ya kufungiwa maisha kutojihusisha na soka, leo ametinga kwenye ofisi za TFF, Karume Ilala ikiwa ni siku chache tu zimepita tangu Mahakama imrejeshe katika nafasi yake.
Wambura amefika ofisni hapo kwa lengo la kuripoti na kutoa taarifa ya mahakama kuwa sasa amerejea rasmi kazini lakini hajawakuta viongozi wa juu zaidi ya wahudumu wa kawaida.
''Nimefika hapa na barua yangu ambayo ilitolewa na mahakama na kutumwa TFF kuwa nirudishwe kazini na imepokelewa TFF na ikasainiwa kwahiyo leo nimekuja na itambulike kuwa nimeshaanza kazi tangu Novemba 30 siku ambayo uamzi wa mahakama ulitolewa'', amesema Wambura.
Hata hivyo Wambura amesema licha ya kutowakuta viongozi wa juu, lakini yeye atafanya kazi kama kawaida kwasababu hakufungiwa kuwa makamu wa Rais bali alifungiwa kujihusisha na soka na uamzi huo umetenguliwa kwahiyo yupo huru kuendelea na nafasi yake.
Aidha amesisitiza kuwa endapo hawatampa ushirikiano atarudi mahakamani kwenda kutoa taarifa kuwa maamuzi ya mahakama hayajatekelezwa.
Wambura alifungiwa maisha kutojihusisha na soka, Machi 15, 2018, siku 10 kabla ya Machi 25, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilipomteua Athumani Nyamlani kukaimu nafasi hiyo ya makamu wa rais wa TFF.