Wananchi wa Congo Wapiga Kura Kumchagua Rais Mpya


Raia wa DRC wapigakura Jumapili hii katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kupelekea mabadilishano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya kidemokrasia tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1960.

Rais Joseph Kabila, ambaye amekuwa madarakani tangu kuuawa kwa baba yake mnamo mwaka 2001, ataachia ngazi katika hatua ya kihistoria kwa taifa ambalo limeshuhudia utawala wa kiimla, mapinduzi ya kijeshi na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu lilipopata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Kukubali kwake kuheshimu ukomo wa mihula kunawakilisha hatua mbele kwa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini. Wakosoaji hata hivyo, wanasema huenda uchaguzi huo ukakumbwa na udanganyifu, na kwamba Kabila huenda akaendelea kutawala kupitia nyuma ya pazia. Hajaondoa uwezekano wa kuwania tena urais mwaka 2023.

Licha ya kuahirishwa mara kwa mara kwa uchaguzi huo ambao awali ulipaswa kufanyika mwaka 2016, wanadiploamsia na waangalizi wa uchaguzi wanasema serikali haijafanya maandalizi ya kutosha, na kuibua wasiwasi wa kurudiwa kwa vurugu zilizofuatia uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011.

Vikosi vya usalama vimeua zaidi ya nusu dazeni ya wafuasi wa upinzani kwenye kampeni na maandamano ya vurugu yaliripuka wiki hii baada ya maafisa kutangaza kuwa ngome tatu za upinzani, zinazochangia wapigakura milioni 1.2 kati ya jumla ya wapigakura milioni 40 nchini kote, hazitaweza kushiriki uchaguzi kutokana na hatari za kiafya zinazosababishwa na mripuko unaoendelea wa Ebola na vurugu za kikabila.

Wanadiplomasia wa kigeni waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba karibu asilimia 60 tu ya vifaa vya kupigia kura vilikuwa vimewasilishwa nchini kote, na waangalizi wa uchaguzi wamesema vituo vya kupigia kura katika mji mkuu Kinshasa vitapambana kuwahudumia wapigakura wote wakati wa muda wa kupiga kura, unaoanza saa 12 asubuhi hadi saa 11 jioni.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad