Watalii watatu wa Vietnam na mwongozaji utalii mmoja wameuwawa Ijumaa, baada ya bomu lililotegwa kando ya barabara kuripukia basi lililokuwa likifanya safari yake kuelekea kwenye mapiramidi ya Giza nje ya mji wa Cairo.
Taarifa ya mwendesha mashitaka wa umma imesema watalii 11 kutoka Vietnam na dereva wa basi raia wa Misri, walijeruhiwa wakati bomu hilo lililotengenezwa nyumbani kuripuka. Bomu hilo lilitegwa karibu na mtaa wa Mariyutiya katika wilaya ya Al-Haram karibu na mapiramidi ya Giza.
Basi hilo lilikuwa limewabeba jumla ya watu 16 wakiwemo watalii 14, dereva na mwongoza utalii raia wa Misri. Vikosi vya usalama vilisambazwa kwa haraka katika eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi.
Waziri mkuu Mostofa Madbouli aliwatembelea watalii waliojeruhiwa hospitalini, ambako alitangaza kwamba mwongoza utalii alifariki kutokana na majereha aliyoyapata. Madbouli alitoa wito wa "kutokuza" tukio hilo akisisitiza kwamba "hakuna nchi inayoweza kuhakikisha usalama wa asilimia 100".
"Inawezekana wakati wowote tukio moja likatokea hapa au pale", Madbouli aliwaeleza waandishi wa habari. Hapakuwa na kundi lililodai kuhusika na tukio hilo. Baadae, Marekani ilitoa taarifa ya kulaani shambulio hilo.
"Tunaungana na Wamisri wote katika vita dhidi ya ugaidi na kuunga mkono serikali ya Misri katika kuwachukulia hatua wahusika wa shambulio hili", alisema naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Robert Palladino.
Sekta ya utalii ya Misri imekuwa ikihangaika kujifufua kutoka katika mashambulio ya kigaidi na ukosefu wa usalama wa ndani ambao umeshuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni. Mnamo Julai 2017, watalii wawili wa Kijerumani walichomwa kisu hadi kufa na wanajihadi katika eneo la kitalii la Hurgada nchini humo.
Mwezi Oktoba 2015, shambulio la bomu lililodaiwa kutekelezwa na kundi lenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiisslamu IS liliwaua watu 224 waliokuwemo katika ndege ya abiria iliyokuwa imewabeba watalii wa Urusi kwenye rasi ya Sinai.
Sekta ya utalii imeanza kustawi tena. Kwa mujibu wa takwimu watalii waliowasili nchini Misri mwaka 2017 walifikia milioni 8.2 kutoka milioni 5.3 mwaka mmoja uliopita. Zaidi ya wanajihadi 450 na karibu askari 40 wa Misri wameuawa tangu mashambulizi yalipoanza, kwa mujibu wa jeshi. Mapiramidi ya Giza ndio pekee yaliyosalia miongoni mwa maajabu saba ya mambo ya kale na kivutio kikubwa kinachovutia wageni wengi kutoka duniani kote.
Tukio hili litachochea mamlaka kuimarisha usalama zaidi katika maeneo ya makanisa na yenye mikusanyiko mikubwa kuelekea kilele cha sherehe za mwaka mpya, pamoja na sikukuu ya Krismasi ya madhehebu ya Coptic ya Kiorthodox. Kwa zaidi ya miaka miwili, mashambulizi ya wanamgambo dhidi ya makanisa nchini Misri yamekuwa yakilenga makanisa au mabasi yaliyowabeba mahujaji kuelekea jangwani, na kuwaua mamia ya watu.
Watalii Wauawa kwa Bomu karibu na Mapiramidi ya Misri
0
December 29, 2018
Tags