Watu Wanne wa Familia Moja Wapigwa Risasi askari wa Wakala wa Hifadhi wa Misitu (TFS)

Watu Wanne wa Familia Moja Wapigwa Risasi askari wa Wakala wa Hifadhi wa Misitu (TFS)
Ndugu wanne wa familia moja katika Kijiji cha Ikongwe, Kata ya Sitalike wilayani Mpanda, wamelazwa Hospitali ya Mkoa wa Katavi, baada ya kudaiwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za miili yao na askari wa Wakala wa Hifadhi wa Misitu (TFS) wa Halmashauri ya Nsimbo.

Diwani wa Kata ya Sitalike, Adamu Cherehani  jana alisema tukio hilo lilitokea juzi saa sita mchana na kuzua hataruki kubwa kutoka kwa wananchi.

Aliwataja wanakijiji waliopigwa risasi kuwa ni Josephat Patrick (27) aliyepigwa risasi mbili kifuani, Jofrey Patrick (39),aliyejuruhiwa mkono wa kushoto,Fiberiti Patrick (40), alijeruhiwa mguu wa kushoto, Januari Patrick (22), alipigwa risasi ya bega la kulia na mwingine aliyetambulika kwa jina la Nkuba Sai aliyepigwa risasi mkono wa kushoto .

Diwani Cherehani, alidai chanzo cha wanakijiji hao kushambuliwa kwa risasi ni askari wa TFS waliofika kijijini na kuanza kufyeka mahindi yao kwenye mashamba kwa kile walichodai yamelimwa ndani ya eneo la hifadhi ya Msitu wa Msaginya .

Baada ya kupata taarifa mahindi yao yanafyekwa, wanakijiji hao waliokuwa zaidi ya kumi walifika mashambani na kuwasihi askari hao waache kufyeka mazao yao kwa sababu ndiyo wanategemea kwa chakula na familia zao, lakini waliwagomea.

Alisema askari waliendelea kufyeka mahindi hayo, hali ambayo iliwafanya wanakijiji waanze kuwazomea.

“Haya mahindi yalikuwa yamebakiza mwezi mmoja tu yaive, lakini askari wamefyeka yote, jambo hili linatia uchungu,”alisema.

Kutokana na hali hiyo, wananchi walianza kuwazomea askari hao wakati wanaingia kwenye gari lao aina ya Toyota LandCruser, ghafla wakaanza kurusha risasi ovyo.

Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM) alisema amesikitishwa na kitendo hicho kwani hawakuwa na sababu ya kutumia nguvu kubwa kiasi hicho kuwakabili wananchi ambao hawakuwa na silaha.

Alisema eneo hilo linalodaiwa mali ya TFS, lilipimwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2002 na kutenganisha maeneo ya hifadhi na shughuli za binadamu

Alisema eneo hilo lilipimwa tena mwaka huu chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda kabla ya kuanzishwa Halmashauri ya Nsimbo .

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema hatua zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

Alisema alikwenda eneo hilo la tukio kuokota ganda moja la risasi ambayo inaonekana kuwa ni gobore.

Alisema ameagiza kukamatwa mara moja kwa askari wa TFS waliohusika kufanya kitendo hicho ili waweze kuhojiwa na sheria kuchukua mkondo wake wake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad