Waziri Jafo: Mabosi Wengine Wana Roho Mbaya Kama Nyoka


Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amesema kuna baadhi ya watumishi na viongozi serikalini wana roho mbaya kama nyoka.

Amesema kuna baadhi ya watumishi ambao wamekuwa wakijijali wenyewe kuliko watumishi walioko chini yao na kusisitiza kuwa kama wapo katika wizara yake washindwe na walegee.

Aliyasema hayo juzi wakati wa utoaji tuzo ya utumishi iliyotukuka kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mussa Iyombe, iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica).

“Tuwe na upendo, tusiwe na tabia ya nyoka, maana nyoka namfahamu hata akiwa mfupi au mrefu lakini roho yake mbaya atamgonga nyati, kumla hawezi lakini basi tu,” alisema Jafo na kusababisha watu kuangua kicheko.

Jafo alisema kuna baadhi ya watumishi wanafanya mambo ya aibu na kuna baadhi ya mabosi wanaposafiri na madareva wao kwenda mikoani, wanakaa na pesa za mafuta badala ya kuwakabidhi madereva.

Alisema pindi mafuta yanapoisha mabosi hao ndipo wanatoa pesa na kuwapa madereva, lakini jambo la kushangaza wakati wa kufanya marejesho ya pesa madereva ndio wanahusika.

“Leo hii Katibu Mkuu (Iyombe) kuna watu wanafanya mambo ya aibu. Utakuta dereva wa kawaida unatoka naye safari hapa unaenda Geita. Mmetia saini pesa ya mafuta na posho lakini pesa ya mafuta ya dereva anakaa nayo bosi,” alisema na kuongeza:

“Yaani hadi taa ya mafuta inawaka dereva anachanganyikiwa anamuuliza bosi, bosi mafuta yameisha, bosi anaingia mfukoni anatoa pesa na kumpa dereva akanunue mafuta wakati pesa ya mafuta ametia dereva halafu retirement (ujereshaji masurufu) anafanya dereva. Hiyo ni roho mbaya iliyopitiliza katika maisha ya binadamu na mimi nasema kama hao watu wapo ofisini kwangu washindwe na walegee,” alisema Jafo.

Jafo alisema kuna baadhi ya idara ambazo watumishi wadogo wasiokuwa na sauti wananyimwa fursa pindi zinapotokea, huku baadhi ya watumishi wakipendelewa kwa kupewa fursa mara kwa mara na mabosi.

“Lakini kuna idara zingine watu wadogo kabisa wasiokuwa na sauti hata fursa ananyimwa, inatakiwa mtu apewe fursa achangamke, mtu anakuwa na watu wake hao hao anaowapa fursa, unakaa na watu ofisini watu wanamawazo wanaona kama wametengwa wanamsongo wa mawazo, hili ni jambo baya zaidi,” alisema.

“Jambo kama hili ndilo linasababisha watu wanakuwa na matabaka, kero, machungu, nendeni mkawe wema,” alisema Waziri Jafo.

Waziri Jafo aliwataka watumishi kubadilika na kuwa na roho nzuri na wanapaswa kujifunza kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara yake Musa Iyombe.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad