Waziri Majaliwa: Serikali Imetoa Kipaumbele Matumizi ya Tehama Nchini

Waziri Majaliwa: Serikali Imetoa Kipaumbele Matumizi ya Tehama Nchini
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku.



Hivyo, amewataka wananchi kutumia vizuri teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano kwenye shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta mbalimbali kwa lengo la  kukuza uchumi na kuwapunguzia wananchi umaskini pamoja na kuongeza ajira.



Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Desemba 5, 2018) katika sherehe za utoaji tuzo za mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kuwaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini.



“Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache. Ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema zikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo. Na kwa wataokiuka sheria ipo na inaendelea kufanya kazi.”

Amsema Serikali inaamini kuwa matumizi ya TEHAMA yataongeza ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti kwa wakati mmoja.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Matumizi ya TEHAMA kwa kiasi kikubwa yatapunguza gharamaza za uendeshaji kwani yanaweza kufanikisha mawasiliano binafsi, warsha na maelekezo mbalimbali kuwafikia walengwa bila ya kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi.”

Ametoa mfano Juni 2017 Rais Dkt. Magufuli alizindua mfumo wa ukusanyaji Mapato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwa njia ya kielektroniki na kudhihirisha kuwa, sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni muhimili muhimu wa maendeleo kwenye sekta zote, ikiwemo viwanda, utalii, ujenzi, elimu, afya, kilimo, uvuvi na ufugaji.

“Kwa kuzingatia hayo, mwezi Juni 2018 wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Serikali ilizindua mifumo tisa ya TEHAMA, ambayo inalenga kuimarisha utendaji wa Serikali hususan katika kuwahudumia wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, ukusanyaji mapato na utoaji wa taarifa.”



Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kutekeleza kwa vitendo azmaya kuwapatia wananchi maendeleo hususani waishio maeneo ya vijijini huduma bora na kwa wakati.

Amesema kwa sasa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inauwezo wa kuona na kubaini makusanyo yanayoendelea kukusanywa katika halmashauri mbalimbali nchini na kiasi kinachoingizwa benki kwa kupitia TEHAMA.

Pia, Waziri Mkuu amsema Serikali imeendelea kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye taasisi zake ili kufanikisha azma ya kutumia Serikali mtandao, zoezi ambalo linakwenda sambamba na kuunganisha baadhi ya shule za msingi, shule za Sekondari, Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Polisi, Hospitali za Wilaya, Vyuo Vikuu na Vituo vya Posta.

Wakati huo huo,Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya HUAWEI kwa uzinduzi wa program yao ya Seed of the Futureambayo inalengo la kuwajengea uwezo wa TEHAMA wanafunzi mbalimbali nchini katika hatua za awali kabisa.

Amesema iwapo TEHAMA itatumika vizuri itatoa fursa kwa watu wote kupata elimu, kuleta usawa katika elimu, kujenga mazingira na mbinu bora za ufundishaji na kujifunza, kuongeza weledi wa walimu, kuimarisha usimamizi wa masuala ya elimu, uongozi na utawala.

Mashindano hayo ya TEHAMA ya HUAWEI yaliasisiwa mwaka 2015 na baadaye mwaka 2016 yakazinduliwa huko Afrika Kusini, ambapo hadi kufikia mwaka 2017 tayari wanafunzi wapatao 40,000 wameshiriki mashindano hayo.

Kwa upande wa Tanzania, yamezinduliwa mwaka huu, ambapo wanafunzi 500 walishiriki na baadaye kubaki 50, ambapo  waliokabidhiwa tuzo ni saba na watatu kati yao na mkufunzi mmoja wamepata fursa ya kushiriki hatua inayofuata ya mashindano hayo nchini Afrika Kusini.

Sherehe hizo zimehudhuliwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Balozi Wang Ke, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Wazri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, Mkurugenzi Mtendaji wa HUAWEI Tanzania Frank Zhou na wawakilishi mbalimbali wa taasisi za Umoja wa Mataifa nchini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad