Waziri Mhagama: Kilimo biashara kuwakomboa vijana Kiuchumi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amesema serikali imedhamiria kuwezesha vijana kiuchumi kupitia kilimo biashara ili kuchochea ongezeko la ajira na kipato.

Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji, wilayani Kigoma wameanza kutekeleza mradi unaolenga kuwezesha vijana kushiriki katika shughuli za uchumi kupitia mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali kwenye kilimo na ufugaji.

Akizungumza katika ziara yake mkoani Kigoma wakati wa kukagua shughuli za utekelezaji za TNBC, Mhagama alisema vyombo hivyo vimeanza utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na Chuo cha Maendeleo Kihinga.

“Nitoe wito watendaji wa halmashauri na ngazi ya mkoa wa Kigoma waendelee kuwaunga mkono vijana hawa wanaoshiriki katika mradi huu wa kilimo biashara. Nawataka mtambue haya yote yanafanyika kwa sababu ya jitihada zinazofanywa na serikali, hivyo ufadhili wa mradi huu unaunga mkono jitihada zake za kuwezesha vijana,” alisema.

Naye Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (masuala ya majadiliano ya sekta ya umma na binafsi), Andrew Mhina, alibainisha kuwa katika kuhakikisha unawawezesha vijana kuwa na ujuzi wa kilimo na ufugaji utakaowawezesha kujiajiri, wameanza ufadhili wa awali kwa kutoa Sh.  milioni 53 ambazo zimetumika katika ujenzi wa mabwawa ya samaki, ukarabati wa mabanda ya kufugia kuku na kuandaa shamba darasa.

 Mradi wa kuwezesha vijana kushiriki katika Kilimo Biashara wilayani Kigoma, unasimamiwa na kutekelezwa na Ofisi ya Rais (Tamisemi) kupitia Manispaa ya Kigoma, Chuo cha Maendeleo Kihinga, Chuo cha Uvuvi Kigoma, Mradi wa LIC na Baraza la Biashara la Wilaya ya Kigoma.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad